Fidelis Butahe na Suleiman Msuya
Rais John Magufuli |
UAMUZI wa Rais John Magufuli kutengua
uteuzi wa rafiki yake, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ni
wa tatu tangu aunde Serikali, sasa analazimika kukuna kichwa kuteua waziri
mwingine kushika nafasi hiyo.
Wakati hilo likisubiriwa, wanasiasa na
wasomi wameieleza JAMBO LEO kuwa hakuna waziri atakayeteuliwa na kusalimika
katika wizara hiyo, kwa madai kwamba inazungukwa na rushwa kubwa za kimataifa, mikataba
mibovu na kuingiliwa uamuzi na Ikulu.
“Ndiyo maana tumekuwa tukipendekeza
kugawanywa kwa wizara hii kwa maana ya kuwa na wizara mbili; ya Nishati na ya Madini,”
alisema Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema.
Mei 20 mwaka jana, kwa mara ya kwanza Rais
alitengua uteuzi wa rafiki yake mwingine wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles
Kitwanga na nafasi yake kuzibwa na Mwigulu Nchemba, ambaye awali alikuwa Wizara
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, huku Mbunge wa Buchosa, Dk Charles Tizeba
akiteuliwa kuchukua mikoba ya Mwigulu.
Mabadiliko ya pili ya Baraza la Mawaziri
yalifanyika Machi 23, baada ya mkuu huyo wa nchi kumteua Dk Harrison Mwakyembe
kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuchukua nafasi na Nape
Nnauye ambaye aliachwa.
Katika mabadiliko hayo, Profesa Palamagamba
Kabudi ambaye awali aliteuliwa na Rais kuwa mbunge, alipewa Wizara ya Katiba na
Sheria ambayo kabla ya mabadiliko hayo ilikuwa ikiongozwa na Dk Mwakyembe.
Rais hakusubiri Profesa Muhongo ajitathmini,
baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi wa sakata la kiwango cha madini kwenye
kontena, alikiri kuwa na urafiki na Mbunge huyo wa Musoma Vijijini na hilo
halikumfanya asite kumwajibisha, kwani baada ya kuisoma ripoti hiyo, Ikulu
ilituma taarifa kwa vyombo vya habari ikieleza kuwa Rais ametengua uteuzi wa
mtaalamu huyo wa miamba.
Mara zote mbili alizofanya mabadiliko ya
Baraza la Mawaziri, Rais Magufuli amekuwa na utaratibu wa kuhamisha mawaziri
kutoka wizara moja kwenda nyingine au kuteua wabunge na kuwapa wizara.
Katika mabadiliko hayo mawili aliyofanya,
ni Dk Tizeba pekee ambaye aliteuliwa kuwa waziri kutoka miongoni mwa wabunge wa
majimbo.
Iwapo Rais Magufuli atazingatia
utaratibu wa mtangulizi wake Jakaya Kikwete kuteua waziri kutoka mkoa ambao
waziri aliyeondoka anatoka, huenda nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Muhongo
ikajazwa na wabunge kutoka mkoa wa Mara.
Baadhi ya wabunge wa CCM kutoka mkoani
Mara ni Boniface Getere (Bunda Vijijini), Nimrod Mkono (Butiama), Vedastus
Mathayo (Musoma Mjini), Kangi Lugola (Mwibara) na Lameck Airo (Rorya).
Pia, kauli ya CCM jana kwamba imechoshwa
na mauaji yanayotokea kila uchwao mkoani Pwani, ni sawa na kutuma ujumbe kwa
Rais Magufuli kwamba kuna tatizo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
kuchochea ukubwa wa mabadiliko.
Utaratibu
Miongoni mwa wateule wake ni Naibu
Spika, Dk Tulia Ackson. Novemba mwaka 2015 Naibu Mwanasheria Mkuu huyo wa
zamani alichukua fomu za kuwania uspika kupitia CCM kabla ya kujitoa dakika za
lala salama kisha akateuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge wa viti maalumu.
Baada ya kujitoa, alijitosa kuwania
unaibu Spika ambapo wabunge 250 walimpigia kura ya ndiyo.
Wengine walioteuliwa kuwa wabunge na
akawapa wizara ni; Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustino Mahiga, Profesa Makame
Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk
Philip Mpango (Fedha) na Dk Abdallah Posi
ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu.
Hata hivyo, Posi aliteuliwa kuwa balozi
kufuatia dosari ya kikatiba katika uteuzi wa wabunge 10 wa kuteuliwa na Rais
ambapo Ibara ya 66 (1)(e) inaeleza katika nafasi hizo, wabunge watano au zaidi wanapaswa kuwa
wanawake. Baada ya kuondolewa Posi, Rais alimteua Anne Kilango kuwa Mbunge.
Hivi karibuni, Rais alimteua Salma
Kikwete kuwa mbunge na kufanya idadi ya wabunge wanawake wa kuteuliwa na Rais
kuwa wanne, kubaki nafasi moja ya uteuzi ambayo ni lazima awe mwanamke.
Mwingine aliyeteuliwa na Rais kuwa
mbunge ni Abdlallah Bulembo na kufanya idadi ya wabunge walioteuliwa na
kiongozi mkuu huyo wa nchi bila kupewa uwaziri kuwa watatu.
Kwa mantiki hiyo, kama Rais Magufuli
atazingatia utaratibu wake wa kuteua mbunge na kumpa wizara, safari hii
atalazimika kuteua mbunge mwingine mwanamke.
Iwapo hatateua na kuamua kubadili
utaratibu wake, huenda Salma na Kilango wakakumbukwa, huku kukiwa na kila
dalili ya baadhi ya mawaziri kuhamishiwa Wizara ya Nishati na Madini.
Wanasiasa, wasomi
Katika maelezo yake, Mbowe alisema
madini yanahusisha mafuta, gesi na vito hivyo vikichanganywa na nishati ni
mzigo mkubwa.
Alibainisha kuwa wizara hiyo inakabiliwa
na vishawishi vingi kutokana na fedha zinazopatikana kwa wawekezaji, jambo
ambalo huwa ni mtego kwa mawaziri.
Huku akikosoa mikataba ambayo Serikali
imeingia na wawekezaji wa sekta ya nishati na madini, Mbowe alisema
ikifuatiliwa kwa undani hakuna atakayebaki salama.
“Yupo Waziri Mkuu mmoja aliondoka kwa
kashfa ya wizara hii. Kusema nani atatosha ni ngumu sana kwa wizara hii,”
alisisitiza Mbowe.
Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK),
Constatine Akitanda aliitaja wizara hiyo na ya Maliasili na Utalii, kukiri kuwa
ni ngumu kuziongoza.
Alidai kuwa mambo mengi yanayoikumba
nchi kwa sasa ni matokeo ya nchi kuingia mikataba mibovu, hasa katika utawala
wa Serikali ya Awamu ya Tatu.
“Tunachopaswa kufanya ni kuangalia mfumo
na mikataba iliyoingiwa. Imetawaliwa na nguvu ya pesa, hakuna waziri
atakayekuwa salama,” alisema Akitanda.
Kwa upande wake, kada wa Chadema na
mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema:”Madini na nishati ni
rasilimali zinazoongozwa kwa rushwa duniani, ni ngumu kutulia.”
Kafulila alisema nchi kadhaa duniani
zinapigana kwa sababu ya nishati na madini, jambo alilodai kuwa linaakisi
nchini.
Rais wa zamani wa Chama kilichofutwa cha
APPT-Maendeleo, Peter Mziray alisema, “Kama Mkapa angeona mbali haya mambo
yasingetokea hivi sasa. Alishiriki ubinafsishaji ambao umenufaisha wageni.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM) Dk Frank Tilly alisema kinachoikumba wizara hiyo ni
matokeo ya nchi kukosa muundo madhubuti wa uongozi, kusababisha viongozi
kufanya mambo wanavyojisikia.
0 comments:
Post a Comment