Mwandishi Wetu
Hamad Yusuph Masauni |
MBUNGE wa Jimbo la Konde, Khatib Said
Haji amemtaja Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani, Hamad Yusuph Masauni, kuwa ni mmoja wa watu aliodai wanasababisha mgogoro
ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).
Isitoshe, akasema hawakumuacha Profesa
Ibrahim Lipumba ila walilenga Watanzania kutambua anayofanya na vibaraka wake.
Haji alisema hayo wakati akichangia bajeti
ya wizara hiyo ambayo iliwasilishwa na Waziri Mwigulu Nchemba bungeni jana.
Mbunge huyo alisema Masauni amekuwa
akishirikiana na kundi la CUF kuhakikisha anakiua chama hicho lakini hatafanikiwa.
Alisema mkakati wa Masauni na kundi la
Mungiki ni kuona damu inamwagika ili kukifuta chama hicho.
“Watu wetu, viongozi wetu wameonesha
uvumilivu mkubwa. Je, kama juzi yule mpuuzi ambaye alikamatwa pale
zisingekuwepo busara zetu si angeuawa, sisi tumedhamiria kulinda amani ya
nchi,” alisema.
Haji alisema CUF haimuogopi Lipumba na uwezo
wa kumnyoosha wanao. Nia wanayo na nguvu wanayo na wanaweza kutekeleza hilo
wakati wowote kama watataka.
Alisema asilimia kubwa ya Watanzania
wamebaini upungufu wa Lipumba jambo ambalo linawapa faraja mwisho wake unafika.
Pia alizungumzia sakata la mlundikano wa
mahabusu ndani ya magereza kuwa ni moja ya changamoto ambayo inatakiwa kutatuliwa.
Mbunge huyo alitoa mwito kwa Serikali
kuondoa watu ambao hawahusiki ili kuondoa msongamano magerezani.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tandahimba, Katani
Katani (CUF), alisema migogoro ndani ya vyama vya siasa inachochewa na Jeshi la
Polisi kwa kuwa kigeugeu katika maamuzi yake.
Mbunge huyo alitolea mfano kuhusu
kufanyika mkutano wa ndani wa chama hivi karibuni ambapo Mwenyekiti wa Kamati
ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro ambaye alizuiwa kufanya mkutano wa ndani mkoani
Tanga.
Alisema kinachoendelea ni ishara tosha
kuwa Jeshi la Polisi linatumika hali ambayo inaweza kusababisha mgogoro ndani
ya nchi.
Katani alisema kitendo cha Waziri
Mwigulu kushindwa kusimamia haki katika suala dogo la CUF ni ishara tosha kuwa
hata nafasi ya urais ambayo aliiomba alikuwa hatoshi.
“Sisi ni binadamu itafikia mahali
uvumilivu utafikia mwisho kwani ambayo yanafanyika hayatendi haki kwa watu
wote,” alisema.
Mgogoro wa CUF umedumu takriban miezi
sita sasa ambapo Lipumba na kundi lake linavutana na kundi lingine ambalo
linatambulika kuwa ni la Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuhusu
uhalali wa Lipumba kurejea katika nafasi ya uenyekiti.
0 comments:
Post a Comment