Mwandishi Wetu, Dodoma
WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Ardhi na
Maji, wameshauri Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT),
kutanua wigo wa shughuli zake ili
wakulima wengi wadogo wanufaike nje ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mjini Dodoma, wajumbe walipokea taarifa ya
shughuli zinazofanywa na SAGCOT kwa lengo la kujua changamoto ambazo shirika hilo
linakabiliana nazo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William
Ole Nasha aliwakaribisha wajumbe hao na kusisitiza kuwa wao ndiyo sauti ya
SACGOT.
"Naamini Kamati hii ya Bunge itapata taarifa ya
shughuli za SACGOT na hivyo kuwa katika nzuri ya kuilezea,"alisema.
Mwenyekiti wa Kamati, Dk. Mary Nagu, amesema amevutiwa na
juhudi za SAGCOT katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hali inayoonyesha
wakulima wadogo sasa wana fursa nyingi za kujinufisha kupitia kilimo kinyume na
mazoea kuwa kilimo ni shughuli ya watu wa chini.
“Naona hata hiki kikao kimekuwa kifupi naomba tuandae
kingine ili tupate elimu zaidi kuhusiana na shughuli mnazofanya kuwaamsha
wakulima na kuona fursa, vilevile tutajipanga kamati tutembelee kongani
mlizoainisha ili tuangalie namna mazao yanavyolimwa na njia zinazotumika
kuongeza uzalishaji.
“Kingine nilichojifunza ni fursa za wafanyabiashara na
wawekezaji kupitia kilimo, ni wazi wawekezaji wanategemea kwa kiasi kikubwa
mavuno na mazao bora ili kuzalisha bidhaa nzuri. Uchumi wa viwanda unategemea
kilimo chenye tija na nyinyi mnatuhakikishia kuwepo tija hiyo,” alisema Dk.
Nagu.
Wajumbe walitaka ziwepo njia nzuri za kuhifadhi mazingira
ili kupata maji ya uhakika siku zote na udongo wenye rutuba kwa ajili ya kilimo
bora.
Wameishauri SAGCOT
kuongeza elimu juu ya namna bora ya kutunza mazingira katika kongani
wanazofanyia kazi.
Awali akiwasilisha taarifal ya Sagcot juu ya shughuli
zake, Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Bwana Geoffrey Kirenga, amesema lengo lao
kubwa ni kubadili sekta ya kilimo kutoka kilimo cha mazoea na kuwa kilimo cha
biashara pamoja na kuongeza uzalishaji kwa wakulima wadogo.
Alisisitiza mambo wanayoyaangazia katika kongani kuwa ni
kudhibiti matumizi ya maji na ardhi, kuongeza uzalishaji wa mazao katika
hekta. Suala lingine ni kuongeza
mnyororo wa thamani katika mazao ili kupata faida na kukuza uchumi wa nchi
kupitia kilimo.
“Tulipoanzisha mpango huu miaka sita iliyopita tulikuwa
na mipango mingi na baadhi imeshaanza kuzaa matunda. Kutokana na mafanikio tuliyopata, tunatazamia kuwatoa katika umasikini zaidi ya
watu milioni mbili.
Hadi kufikia 2030 Sagcot inatwania hekta 350,000
zizalishe mazao ya kilimo kwa faida “na tuachane na kilimo cha mazoea ambapo
mkulima faida yote anaitumia kwa ajili ya chakula na mavazi tu.”
Katika kipindi hicho SAGCOT inapanda kuzalisha ajira mpya
420,000 zitokanazo na kilimo. “Hapa tunazungumzia wauzaji pembejeo, wauzaji
bidhaa za kilimo ikiwemo chakula na wakulima wenyewe,” alisema Bw. Kirenga.
SAGCOT imeainisha kongani sita ambazo ni Ihemi
inayojumuisha mikoa mitatu ya Mbeya, Iringa na Njombe, kongani ya Kilombero
inayohudumia Mkoa wa Morogoro, Kongani ya Mbarali (Mbeya na Songwe), Kongani ya
Sumbawanga (Rukwa), Kongani ya Ludewa (Ruvuma) na Kongani ya Rufiji (Pwani).
Hata hivyo kwa sasa kongani inayofanya kazi ni Ihemi
ambayo kwa ujumla wake inasimamia wakulima wa Nyanya, Mchele, Viazi, Soya,
Mahindi na ufugaji kwa ajili ya maziwa. Katika mikoa hiyo kwa ujumla wilaya
sita ndizo zinazoshughulikia kilimo hicho na fugaji ambazo ni Wilaya ya Iringa
Vijijini, Kilolo, Mufindi, Njombe Vijijini,
Wanging’ombe na Njombe Mjini.
Wafadhli wakubwa wa SACGOT ni Serikali ya
Tanzania,Shirika la misaada la Uingereza (UK Aid),Shirika la misaada la
Marekani(USAID),Benki ya Dunia (WBG),Ubalozi wa Norway,Shirika la Maendeleo la
Umoja wa Mataifa (UNDP) na AGRA.
0 comments:
Post a Comment