Kizimbani akidaiwa kuhamisha mali iliyozuiwa


Grace Gurisha

MFANYABIASHARA Erick Lugeleka amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akituhumiwa kuhamisha mali iliyowekewa zuio na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Akisoma hati ya mashitaka jana, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Magela Ndimbo mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa, alidai kuwa mshitakiwa huyo anatuhumiwa kuhamisha umiliki wa mali.

Alidai kuwa Julai 15, 2010 Lugeleka akiwa mmiliki wa nyumba namba 223 kitalu ‘B’ kilichoko Kijitonyama, Dar es Salaam, alihamisha mali hiyo akidai ni ya Yusufu Matimbwa na kukiuka taarifa iliyotolewa na AG, Machi 18, 2010.

Ilidaiwa kuwa Mei 21, 2010 mfanyabiashara huyo alihamisha mali hiyo huku akijua ilizuiwa kwa ajili ya uchunguzi. Baada ya mshitakiwa kusomewa mashitaka alikana kuhusika.

Ndimbo alidai kuwa hajui hatua ya upelelezi ilipofikia kwa sababu hajui jalada liliko, hivyo kuomba kesi hiyo ipangwe tarehe nyingine ya kutajwa, ili apate muda wa kufuatilia hatua ya upelelezi na pia alidai hana pingamizi na dhamana.

Hakimu Nongwa alisema ili mshitakiwa awe nje kwa dhamana anatakiwa awe na wadhamini wawili, kila mmoja asaini dhamana ya Sh milioni 10 na wawe na anuani za kuaminika.

Hadi gazeti hili linaondoka eneo la Mahakama, mshitakiwa alikuwa hajadhaminiwa kwa sababu ilidaiwa kuwa wadhamini wake walikuwa njiani kufika mahakamani, hivyo mshitakiwa aliendelea kushikiliwa na Polisi hadi wadhamini wafike.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo