Grace Gurisha
Harry Kitilya na wenzake wawili |
ALIYEKUWA Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Harry Kitilya, na wenzake wawili, leo wanatarajiwa kupandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi inayowakabili
ya uhujumu uchumi itakapotajwa.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Cyprian Mkeha anayeisikiliza, baada ya Hakimu Mkazi Emmilius Mchauru
aliyekuwa akiisikiliza awali kuhamishiwa kwenye Mahakama nyingine.
Awali, upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi
haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ili kuukamilisha, kwa sababu kesi hiyo
ni pana na inahitaji muda wa kupeleleza kwa sababu upelelezi utatakiwa
kufanyika nje ya nchi.
Kitilya na wenzake wanaendelea kuwa rumande, ambapo hivi
sasa wanatimiza mwaka mmoja gerezani kwa sababu ya upelelezi kutokamilika na pia
wanashitakiwa kwa kutakatisha fedha, hivyo kisheria kukosa dhamana.
Mbali na Kitilya, wengine aliyekuwa mlimbwende wa
Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na aliyekuwa mwanasheria wa benki ya Stanbic
Tanzania, Sioi Solomon.
Kitilya na wenzake walipandishwa kizimbani mara ya kwanza
kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Aprili mosi, mwaka jana
wakishitakiwa kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kughushi na
kutakatisha fedha haramu.
Tangu siku hiyo kila kesi hiyo ikija mahakamani, upande
wa Jamhuri umekuwa ukiiambia Mahakama kuwa upelelezi haujakamilika na kuomba
tarehe nyingine ya kutajwa, ambapo mawakili wa washitakiwa hao wamekuwa wakipiga
kelele kuhusu wateja wao kusota gerezani.
Hali hiyo ilisababisha, Wakili Alex Mgongolwa kuomba
wateja wake waachwe huru, na wakishakamilisha upelelezi ndipo wakamatwe tena
kuliko kukaa gerezani bila sababu, baada ya kushindikana hilo, wakaomba Serikali
iwaeleze hatua waliyofikia, lakini bado hawajaeleza.
Awali, upande wa mashitaka ulidai mahakamani kuwa katika
tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013 Dar es Salaam, washitakiwa hao
watatu walipanga kwa kushirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa
mahakamani hapo, kutenda kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka
serikalini.
Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 kwenye makao makuu
ya Stanbic Tanzania Limited, Kinondoni, Sinare akiwa na nia ovu, alighushi taarifa
ya maombi ya fedha ya benki ya Standard ya Agosti 2, 2012.
0 comments:
Post a Comment