IKIWA imebaki miezi takribani mitano
kabla ya kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba wanafunzi 33 wa shule ya msingi
ya Lucky Vincent ya Arusha wamepoteza maisha katika ajali ya gari, tukio ambalo
linarejesha kumbukumbu za ajali zilizotikisa Taifa na kuacha simanzi kubwa.
Wanafunzi hao, walimu wawili na dereva wa
shule hiyo walikufa Mei 6 eneo la Rotya wilayani Karatu wakienda kufanya
mtihani wa ujirani mwema na shule ya Tumaini Junior Academy.
Unaweza kujiuliza maswali mengi kuhusu ndoto
za wanafunzi hao waliokuwa na umri wa kati ya miaka 12 na 15 zilivyoyeyuka kama
mshumaa. Vipi kuhusu wazazi na walezi wao? Hakika ni msiba usioelezeka.
Tangu mwaka ulipoanza, Taifa
limeshuhudia matukio yatokanayo na majanga ya asili, uhalifu, hata ya kisiasa
na mengine mengi ya utendaji wa kila siku wa Serikali, lakini ajali ya
wanafunzi hao ni tukio lililotikisa kutokana na kuhusisha watoto waliokuwa na
ndoto za kuitumikia Tanzania, huku wakitegemewa na wazazi wao.
Ajali ya wanafunzi hao ina mwelekeo wa
kufanana na ya sekondari ya Shauritanga ambayo mabweni yake yalishika moto na
kusababisha vifo vya wanafunzi zaidi ya 40.
Yafuatayo ni baadhi ya matukio ya ajali
yalitokea nchini na kuacha simanzi kwa wananchi:
Juni 18, 1994
Wanafunzi zaidi ya 40 wa Shauritanga mkoani
Kilimanjaro walikufa moto, baada ya bweni lao kuungua.
Usiku wa manane, wakiwa wamelala, moto
mkubwa ulizuka. Mabinti hao walipiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa walinzi
lakini hawakufanikiwa hadi wakapoteza uhai wakiwa wamejikusanya sehemu ya
mlango uliokuwa umefungwa na walinzi kwa nje.
Mei 21, 1996
Meli ya mv Bukoba ilizama na kusababisha
vifo vya zaidi ya watu 800. Meli hiyo ilikuwa ikitoka Bukoba na kuzama umbali
wa takriban kilometa 12 kutoka bandari ya Mwanza na inasadikiwa ilikuwa na
abiria zaidi ya 1,200.
Inakisiwa kwamba, watu waliojeruhiwa
katika ajali hiyo walikuwa 100. Mali zilizopotea katika ajali hiyo thamani yake
haikujulikana.
Septemba 9, 2011
Meli ya mv Spice Islander iliyokuwa
ikisafiri kutoka Unguja kwenda Pemba visiwani Zanzibar ikiwa imebeba abiria
2,470 ilizama eneo la rasi ya Nungwi katikati ya mkondo wa bahari na kuua zaidi
ya watu 400 huku 941 wakinusurika.
Aprili 19, 2012
Wasanii 13 akiwamo mwimbaji maarufu,
Issa Kijoti wa kundi la muziki wa taarab la Five Stars Modern Taarab, walikufa
na wengine wanane kujeruhiwa baada ya gari lao aina ya Toyota Coaster walilokuwa
wakisafiria kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam, kupamia lori lililokuwa limeegesha
na kupinduka.
Juni 24, 2002
Ilitokea ajali mbaya ya treni kati ya
stesheni ya Igandu na Msagali wilayani Mpwapwa Dodoma na kuua takribani watu
400, huku zaidi ya watu 700 wakinusurika.
Ajali hiyo ni kati ya matukio
yaliyotikisa Taifa kutokana na mamia ya watu kufa baada ya treni hiyo kushindwa
kupanda mlima na kurudi kinyumenyume umbali wa takribani meta 400.
Julai 18, 2012
Ilizama meli ya mv Skagit wakati imekaribia
bandari ya Zanzibar na hatua za awali za uokoaji zilishindikana hivyo kusababisha
vifo vya mamia ya watu.
Aprili 21, 2014
Watu zaidi ya 20 walifariki dunia na
wengine kujeruhiwa vibaya baada ya basi la Luhuye lililokuwa likitoka Musoma
kwenda Mwanza kuacha njia na kugonga nyumba, kisha kupinduka katika kijiji cha Itimila
wilayani Busega mkoani Simiyu.
Machi 12, 2015
Watu 42 walipoteza maisha na wengine 23
kujeruhiwa baada ya lori la mizigo lililobeba kontena kugongana na basi, ambapo
kontena lililobebwa na lori liliangukia gari hilo la abiria. Ajali hiyo ya aina
yake iliyotokea eneo la Mafinga Changarawe, Iringa.
Watu 37 waliokuwa kwenye basi hilo la kampuni
ya Majinjah Express lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Dar es Salaam, walifariki dunia
hapo hapo na wengine watano kufariki dunia wakiwa hospitali ya Mafinga. Dereva
wa basi na wa lori hilo la kampuni ya Cipex, pia walipoteza maisha.
0 comments:
Post a Comment