Joyce Kasiki, Dodoma
SERIKALI inaangalia
uwezekano wa kuongeza posho ya wazee wa mabaraza ya Mahakama nchi nzima
kutokana na kiwango cha sasa Sh 5,000 kuwa kidogo, pia kupunguza vitendo vya
rushwa.
Waziri wa Katiba
na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbagala, Ali Mangungu (CCM).
Katika swali
lake, Mangungu alitaka kujua kama Serikali haioni kuwa inachochea rushwa kwa
kutoa kiasi hicho kidogo cha posho kwa wazee hao.
Awali katika
swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua kama Serikali haioni ni wakati mwafaka
sasa kuwaongeza posho wazee hao hususan wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar
es Salaam, ambao wamekuwa wakisikiliza kesi nyingi zikiwamo za mauaji.
Akijibu swali
hilo, Profesa Kabudi alisema Serikali itawaongeza posho wazee hao kwa kadri
bajeti itakavyopatikana.
Aidha alisema Serikali
inatambua mchango mkubwa wa wazee wa Baraza katika Mahakama nchini na umuhimu
wa kutoa posho kama motisha na kwamba kutokana na umuhimu huo, ingetamani posho
za wazee hao ziongezeke ili kuendana na hali ya maisha.
Alisema kwa
bahati mbaya posho hizo hutokana na bajeti ya matumizi mengineyo ambazo
hutengwa na Serikali kwa kila fungu.
Hata hivyo Profesa
Kabudi alisema kwa mwaka wa fedha 2016/17, Mahakama ya Tanzania ilitengewa Sh
bilioni 1.27 na mwaka 2017/18 Mahakama imetengewa Sh bilioni 1.85 kwa ajili ya malipo
ya posho ya wazee wa mabaraza.
Alisema Serikali
itaendelea kutenga au kuongeza posho kwa malipo mbalimbali zikiwamo posho kwa
ajili ya wazee hao.
0 comments:
Post a Comment