Mwandishi Wetu
Dk Tausi Kida |
TAASISI ya
Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) imekutanisha wadau wa maendeleo nchini kujadili
bajeti ya Tanzania ya mwaka wa fedha 2016/17 ambao unaelekea ukingoni.
Akizungumza
katika mkutano huo juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk Tausi Kida, alisema
mdahalo huo ni sehemu ya shughuli zinazofanywa na ESRF ili kutazama ni jinsi
gani taasisi hiyo inaweza kuisaidia Serikali kuweka mipango thabiti kwa ajili
ya maendeleo ya nchi.
Dk Kida alisema
mdahalo huo unahusu bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuangalia utekelezaji wa bajeti zilizopitishwa
kwa mwaka wa fedha 2016/17, changamoto zilizopo na nini kifanyike katika bajeti
ya 2017/18.
“ESRF imekuwa ikishirikiana
na wadau ili kuangalia jinsi gani tunaweza kusaidia mchakato wa maendeleo wa
nchi yetu kwa njia ya utafiti, uchambuzi na utayarishaji wa sera na kuongeza
wadau uwezo kupitia mafunzo tofauti,” alisema Dk Kida.
Aliongeza: “Kama
jinsi mnavyojua nchi yetu imekuwa na mipango ya maendeleo inayotekelezwa
kupitia bajeti kwa kuangalia mambo yenye umuhimu kwa Taifa, bajeti imekuwa
ikipangwa kila mwaka kwa kuzingatia maeneo ya kuyapa kipaumbele ili kuleta
maendeleo kwa nchi.”
Mwakilishi wa Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Joviter Katabaro ambaye ni Mkufunzi wa Shule ya Elimu, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, alisema pamoja na Serikali kutoa elimu bure katika
ngazi fulani, lakini bado kuna changamoto katika elimu zinazohitaji kutafutiwa
ufumbuzi katika bajeti ya mwaka 2017/18.
“Pamoja na
jitihada kubwa ya Serikali katika elimu bado kuna upungufu wa majengo 10,000 ya
shule, upungufu wa maktaba 15,000 na vyoo bado havitoshi,” alisema Dk Katabaro.
Profesa Haidari
Amani, Mtafiti Mshiriki Mwandamizi (ESRF) aliyetoa taarifa kuhusu Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi alisema pamoja na sekta ya kilimo kuwa na changamoto, Serikali
inatakiwa kuweka mfumo mzuri kuanzia wakulima wadogo ili kunufaika na kilimo.
0 comments:
Post a Comment