Jemah Makamba
Zitto Kabwe |
MBUNGE wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa
Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema udhibiti wa mapato kutokana kodi
za kimataifa utasaidia kupunguza kodi kwa wafanyakazi nchini.
Aidha, amewashauri wafanyakazi wa
Tanzania, kutambua kwamba wanapaswa kutambua uhusiano chanya kati ya maslahi
yao na aina ya uongozi wa kisiasa kwenye Taifa akiwataka wasikae kando kwenye
harakati za mabadiliko ya kisiasa nchini.
"Jana ni siku yenu katika mwaka.
Kama ilivyo kawaida siku hii husherehekea kwa maadhimisho makubwa ambapo waajiri
Serikali na sekta binafsi hutoa hotuba hivyo ni lazima mzingatie mahitaji
yenu,” alisema.
Alisema pamoja na sherehe hizo, bado
ajira zinazotolewa nchini ni chache ikilinganishwa na idadi ya Watanzania wenye
sifa za kuajiriwa.
Zitto alisema takwimu zinaonesha kuwa ni
wafanyakazi milioni 2.1 sawa na asilimia tisa ya nguvukazi yote ya Taifa.
“Sekta binafsi waliajiriwa wafanyakazi
milioni 1.4 sawa na asilimia 67 na sekta ya umma 700,000 sawa na asilimia 33,”
alisema.
Alisema sekta isiyo rasmi imeajiri
asilimia 91 ya Watanzania, hali ambayo inachangia kukosekana kwa mapato mengi.
Mbunge huyo alisema asilimia kubwa ya
kundi hilo inajihusisha na kilimo, biashara ndogo, uvuvi, ufugaji, uchimbaji wa
madini na utoaji huduma.
Alisema zipo kampuni zinazokwepa kulipa
kodi, hivyo wamiliki wake kujilimbikizia mali nyingi na kuongeza tofauti ya
kipato kati ya wananchi.
Alisema kama hatua madhubuti
hazitachukuliwa tofauti ya kipato itazidi kuongezeka na kuleta hatari kubwa kwa
ustawi wa wananchi na nchi.
"Mwaka 2015/16 kampuni zilichangia Sh
bilioni 773 wakati wafanyakazi walichangia Sh trilioni 2.2 na mwaka 2014/15 yalichangia Sh bilioni 600 na wafanyakazi Sh trilioni 1.9 kama kodi zao
kwenye mapato ya Serikali," alisema.
Alisema ni muhimu Serikali itazame upya
michango ya wafanyakazi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kuwa viwango hivyo
kwa Tanzania viko juu mno na vinapunguza kipato cha mfanyakazi na kuongeza
gharama kwa waajiri.
Zitto pia aliitaka Serikali ifanye
marekebisho ya sheria za kodi zinazohusisha kampuni ya kimataifa ili kuzuia
kumomonyoa wigo wa kodi unaofanywa na
kampuni hizo.
Kuhusu wafanyakazi kutojitenga na siasa
alisema historia inaonesha vyama vya wafanyakazi vina nguvu zaidi ya
kuhamasisha na kuweka mazingira mazuri ya kidemokrasia na utawala wa kikatiba
nchini.
0 comments:
Post a Comment