Grace Gurisha
MADEREVA
wa bodaboda wametoa msimamo wa kutosaidia askari wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama
wa Barabarani wanapopatwa na matatizo.
Wamefikia
hatia hiyo kwa walichodai kuwa wasimamizi hao wa sheria hawana huruma kwani huwatoza
faini bila makosa.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana Dar es Salaam, madereva hao walisema wamekuwa wakitoa
msaada mkubwa askari wanapopata matatizo kazini, lakini wao wamekuwa wagumu kuwasadia
hata kuwasikiliza na kuwabambikia makosa na kuchukua fedha zao kwa rushwa au
faini.
Mmoja wa
madereva hao, Emmanuel Noel alisema askari hao wamekuwa wakiwaonea bila sababu
ya msingi hali inayoendelea kukithiri kwa kasi kutokana na hali ngumu ya
kimaisha sasa, hivyo huona nafuu yao ni kukamata bodaboda.
“Askari
wamekuwa wakigongwa na magari wakiwa kazini, sisi tunafanya jitihada za
kulifukuzia gari hilo hadi kulikamata bila hata kulipwa, wakati mwingine
tunawasafirisha bure tukidhani ni wenzetu, kwani kila siku tuko nao barabarani,
lakini wao hawatuchukulii sisi kama wenzao,” alisema Noel.
Aliongeza:
“Hivi karibuni askari alipigwa kibao na mtu aliyekuwa ndani ya gari wakati
anaongoza magari kwenye mataa ya Tazara, nilimchukua askari huyo na kulifukuzia
gari hadi akalikamata, lakini wao wanashindwa kututhamini sisi, kwa hiyo hakuna
haja nasi kuwathamini.”
Dereva
mwingine, Hashim Omary anayefanya kazi Tabata Kimanga, alisema kila siku Polisi
inawahamasisha wafanye kazi pamoja, lakini askari wamekosa ushirikiano kwao kwa
sababu hata wanapopata tatizo au kufanya kosa, hawawapi nafasi ya kusikilizwa.
Omary
alisema ikitokea wao wamefanya kosa, askari hawataki hata kuwasikiliza, jambo ambalo
si zuri na kwamba trafiki hao walichokiweka mbele ni faini.
“Sijui
ndiyo kutekeleza ile aliyosema Rais wapate hela ya kiwi? Juzi hapa kituoni
kulikuwa na askari, ghafla akaumwa tumbo, nilimchukua hadi hospitali ya Amana, sikumdai
hata shilingi moja, lakini cha kushangaza wao hawana huruma nasi kwa kututoza
fedha bila sababu,” alisema Omary.
Shabani
Zuberi aliomba Serikali kupunguza ugumu wa maisha kwa kuiacha fedha izunguke kwa
sababu maisha yamekuwa magumu na askari wameamua kuponea kwenye bodaboda.
0 comments:
Post a Comment