Shaban Njia, Kahama
WANAFUNZI wa sekondari ya Mwamandi, Msalala wilayani hapa,
wamekuwa wakitumia saa moja darasani huku muda mwingi wakitumia kusomba maji
umbali wa kilometa mbili kwa ajili ya matumizi ya shule.
Hayo yalibainishwa jana na Diwani wa Mwanase jirani na
shule hiyo, Samson Paul katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri
hiyo.
Paul alisema wanafunzi hao wanapokwenda shuleni kusoma
kila siku, walimu huwataka kusomba maji kutoka katika shule ya msingi Mwanase,
hali ambayo husababisha kuhudhuria masomo kwa saa moja tu, kutokana na
foleni kwenye bomba.
Diwani huyo alieleza kuwa mbali na tatizo la maji, shule
hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa walimu. Kuna walimu watatu ambao
wanafundisha zaidi ya wanafunzi 600.
Alisema upungufu huo wa walimu umepunguza kiwango cha ufaulu
kwa kiasi kikubwa, hivyo kuitaka Halmashauri hiyo kuangalia suala hilo na
kulipatia ufumbuzi.
“Sisi wakazi wa Mwananse tunaomba tutatuliwe shida ya
maji hasa kwa wanafunzi wa Mwamandi ambao wanakosa masomo yao. Wanatumia muda mwingi
kusomba maji,” alisema Diwani huyo.
Hata hivyo, alisema tatizo hilo pia linafanya baadhi ya
walimu wanaopangiwa shule hiyo kutoroka kutokana na mazingira magumu.
Mhandisi wa Maji wa Halmashauri hiyo, Cyprian Ndabavunye
alisema Halmashauri imepanga kupeleka
maji kwenye kata hiyo katika mwaka ujao wa fedha, kwani mwaka huu viongozi wa
Kata hiyo walichelewa kuwasilisha bajeti ili kuingizwa kwenye orodha ya miradi
itakayotekelezwa.
“Suala la maji Mwanase, viongozi ndio walichelewa kuleta
bajeti yao lakini tumepanga suala hili kuliweka kwenye bajeti ijayo, kwa hiyo
tunaomba mtuvumilie na tufanye kazi kwa ushirikiano,” alisema Ndabavunye.
0 comments:
Post a Comment