Asha Kigundula, Pwani
HALMASHAURI ya mji mdogo wa Chalinze mkoani
Pwani, imetenga kiasi cha Sh.milioni 36 katika kipindi cha mwaka 2016/2017 kwa
ajili ya kuwalipa posho wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika halmashauri
hiyo.
Kati ya fedha hiyo wenyeviti hao
wanalipwa kila mmoja sh. 30,000 kwa mwezi hadi mwezi July mwaka huu itakapokoma
bajeti hiyo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa
Chalinze, Said Zikatimu alisema halmashauri hiyo imeamua kuwalipa posho
wenyeviti hao kwani wanafanya kazi kubwa ndani ya miaka mitano bila kuambulia
chochote.
Alisema wameshirikiana na mbunge wa
jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete kuona namna ya kuwatupia jicho wenyeviti
hao wa vijiji na vitongoji.
Aidha Zikatimu alieleza kwamba fedha
hizo zitawawezesha wenyeviti hao kujikimu na kuondokana na hali ya kuuza ardhi
za vijiji kwa visingizio vya kukosa posho ama mishahara.
Alibainisha kuwa fedha hiyo pia itaweza
kuwasaidia wenyeviti hao kuwa na morali na ari ya kuchapakazi kwenye maeneo yao
na wamejipanga kila mwaka watakuwa wakitenga fedha hizo.
“Kiasi hiki cha Sh.mil.36 ni fedha
watakazolipwa hadi july 2017 na bajeti inayofuata tutaangalia kama kuna
uwezekanao wa kuongeza kiasi kilichopangwa katika bajeti hii ama ibakie kiasi kilichotengwa
kwenye bajeti hii”alifafanua Zikatimu.
Hata hivyo, Zikatimu alisema wanachotarajia
ni wenyeviti hao kuendelea kuwa wasimamizi wazuri katika vyanzo vya mapato na
kuachana na tabia ya kuuza maeneo ya vijiji kinyume na taratibu.
Alisema wanawahamasisha kusimamia vyanzo
vya mapato ili kuinua makusanyo hasa ya vyanzo vya ndani ikiwemo vizuizi
mbalimbali vya pembezoni na ndani ya mji huo.
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa
halmashauri nyingine nchini kuwaangalia wenyeviti hao kwani kwa Chalinze
imeshaleta tija ndani ya miezi sita tangu kuanza kwa mpango huo.
Aliiomba serikali na halmashauri hizo
ziangalie namna ya kuwatengea fedha wenyeviti wa vijiji na vitongoji kama
ilivyo kwa madiwani na wabunge wanavyotengewa posho wakimaliza muda wao,ili
waweze kuwa na moyo wa kufanya kazi pasipo kukosa chochote.
“Halmashauri ni sehemu ya kwanza na
serikali kuu ni sehemu ya pili,hivyo halmashauri zionyeshe nia ili serikali
ilione hili,kwa kuwapa kipaombele ya kuwatengea fedha bila kuwaacha”
Zikatimu alisema wenyeviti hao
wanasimamia chaguzi mbalimbali na ilani ya CCM hivyo waangaliwe katika suala
hilo ili waweze kujiona ni viongozi wanaoaminika kwenye maeneo yao.
0 comments:
Post a Comment