Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate
maafisa wanne na kuhakikisha wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi ili wajibu
tuhuma za upotevu wa tani 2, 138 za korosho.
Maafisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha
Ushirika cha Masasi (MAMCU), Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Lawrence
Njozi. Wengine ni wakurugenzi wa kampuni
ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Yusuph Namkukula na Ramadhani Namakweto.
Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo kwenye kikao
alichokiitisha Songea mjini jana jioni baina ya watendaji kutoka Bodi ya
Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la BUCO - Masasi na kikundi cha
wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) za wilaya
za Mtwara na Masasi.
Katika kikao hicho, Waziri Mkuu alitaka apatiwe maelezo
ya kina ni wapi zilipo hizo tani 2,138 za korosho wakati taarifa waliyompatia
viongozi hao jana inaonyesha kuwa waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja
ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.
Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU, Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho
zote ziliuzwa na zilishalipwa na wanunuzi wa mnada wa tano, lakini akadai
hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho.
Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Ramadhan Namakweto alikiri
kupokelewa kwa korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni
kwa nini hazionekani zilipo.
“Tangu mnada wa tano, mmekwishafanya minada mingine
mitano hadi kufikia mnada wa 10. Kama kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa
nini korosho za hawa wakulima hazijatolewa ghalani na kuuzwa katika minada
iliyofuata huku taarifa yenu ya fedha kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji
Waziri Mkuu bila kupata majibu ya kueleweka.
Tuhuma zinazowakabili maafisa hao wanne ni kuwalipa kilo
pungufu ya zile zilizowasilishwa ghalani, wakulima wa korosho katika wilaya ya
Masasi na kutowapa maelezo yoyote juu ya upungufu huo.
Nyingine ni kutowalipa fedha kwa wakati wakulima waliouza
korosho kwenye mnada wa tano wa tarehe 10 Novemba 2016 na kutokutoa maelezo
yoyote licha ya kuwa MAMCU ilishauza korosho hizo kwenye minada iliyofuatia na
kupokea malipo.
Nyingine ni kutopelekwa mnadani kwa makusudi kwa tani
2,138 za korosho zilizokuwa katika maghala ya Mtandi na BUCO tangu Novemba 11,
mwka jana; kutokutolewa taarifa ya kuwepo korosho hizo kwa mamlaka husika na
kuwasababishia hasara wananchi.
Tuhuma nyingine ni kushindwa kufuatilia malipo ya korosho
ya tani 1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21,
2016. Korosho hizo zilinunuliwa na Maviga East Africa (tani 503,297); Machinga
Transport (tani 104,200); Tastey (319,576) na Saweya Impex (tani (229,189).
Kutokana na mapungufu hayo, Waziri Mkuu aliagiza watu hao
wapelekwe Masasi chini ya ulinzi ili uchunguzi ufanyike na pia amemuagiza Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU
na kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na kuingia
akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa vyama vya msingi na wananchi
kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada husika.
Mapema,
wakisoma risala yao kwa Waziri Mkuu, wakulima hao walisema wana kero nyingi
sana kama vile kutolipwa fedha zao kwa wakati; kutoeleweka mahali zilipo
korosho ambazo walishaziuza kwa MAMCU, kukatwa makato ya unyaufu ambayo
Serikali ilikwishapiga marufuku na kutosikilizwa malalamiko yao na viongozi wa
MAMCU pamoja na viongozi wa mkoa na wilaya.
“Makubaliano yalikuwa ni kwamba mkulima atapewa fedha
yake siku sita baada ya mnada kufanyika lakini hivi sasa baadhi yetu tumeuza
korosho tangu Oktoba, mwaka jana lakini hadi imefika Januari hii bado
hatujalipwa. Pia kuna makato yaliyoondolewa kwenye mfumo, kwa mfano unyaufu
lakini wao wameyaacha na unapoenda kuuza wanahesabu na kukukata kuwa utalipia
gharama za unyaufu,” alisema msoma risala Bw. Sylvester Mtimbe ambaye pia ni mkulima
kutoka AMCOS ya Chiungutwa.
Wakulima hao wa korosho kutoka Masasi mkoani Mtwara
walikutana Januari 3, 2017 katika kijiji cha Chiungutwa na kuazimia kuwa
wangeandamana hadi Dar es Salaam ili wawasilishe kilio chao kwa Waziri Mkuu au
kwa Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli.
Kwa kutambua umbali uliopo kutoka Masasi hadi Dar es
Salaam na kwamba yeye hakuwepo katika siku waliyopanga kwenda huko, Waziri Mkuu
aliamua kuwaita wakulima hao wamfuate Songea ambako alikuwa na ziara ya kikazi
ya siku nne.
0 comments:
Post a Comment