Zitto ataka marais wastaafu wamshauri JPM



Fidelis Butahe

Zitto Kabwe
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amewashauri marais wastaafu kuishauri Serikali ya Awamu ya Tano kuhusu mambo manne aliyodai yanaashiria taifa kupoteza dira.

Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Isagehe Wilaya ya Kahama mjini.

“Watanzania tumeumbwa na viongozi wetu wameumbwa kuwa wanyenyekevu, ndio maana ninashaangaa Mwinyi (Ali Hassan-Rais wa Awamu ya Pili) yuko wapi?, Mkapa (Benjamin-Rais wa Awamu ya Tatu) yupo wapi? Kikwete (Jakaya-Rais wa Awamu ya Nne) yuko wapi?” alihoji Zitto.

“Kwa nini wako kimya viongozi wastaafu? Wako wapi kuionya Serikali hii …; anayeshindwa kuwa mnyenyekevu mbele ya wananchi waliompa kura?”

Zitto aliyetumia mkutano huo kumnadi mgombea udiwani wa chama hicho, Ibrahim Masele aliyataja mambo hayo manne kuwa ni; kauli ya Rais Magufuli aliyoitoa mkoani Kagera kuwa waathirika wa tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa huo hivi karibuni kila mmoja atabeba mzigo wake, nchi kutonufaika na sekta ya madini na mikataba yake kutowekwa wazi.

Nyingine ni kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa pamoja kukamatwa kwa wabunge wa upinzani, akitolea mfano rufani ya Jamhuri kupinga mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kupewa dhamana. Lema anatuhumiwa kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais Magufuli.

Mikutano ya hadhara

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini ambaye pia alituma hotuba yake hiyo katika vyombo vya habari alisema, “Leo tunaongea na nyinyi kwa sababu kuna uchaguzi mdogo. Mwaka jana mwezi wa sita mkubwa mmoja alikuja na amri ya kuzuia mikutano ya hadhara mpaka 2020…vyama vya siasa vimeundwa na katiba na sheria na inaturuhusu kufanya mikutano.”

“Tusipofanya mikutano ninyi mtajuaje kama chama tawala kinavurunda,? Ndiyo maana ya mfumo wa vyama vingi, lakini bwana mkubwa yule akazuia mikutano na baadhi ya watu wakamuunga mkono.”

Juni mwaka jana Rais Magufuli alipiga marufuku shughuli za kisiasa hadi mwaka 2020, akisema wabunge na madiwani ndio wanaopaswa kufanya mikutano na shughuli nyingine kwenye maeneo yao walimopigiwa kura.

Lakini jana Zitto alisisitiza: “Lakini Mungu nae ana yake kuna kampeni, je atazuia mikutano ya kampeni?”

Zitto alihoji kitendo cha viongozi mbalimbali nchini kutokemea kuzuiwa kwa mikutano hiyo na kusisitiza kuwa mikutano ya hadhara ni haki ya kikatiba, haipaswi kusubiri mpaka chaguzi ndogo.

“…Leo vyakula vimepanda bei ukame unakuja kuna baa la njaa tunasema kwa kuwa kuna uchaguzi mdogo. Kama hakuna (uchaguzi mdogo) mambo haya tusingeyasema?”

Amzungumzia Lema

Kuhusu Lema alisema: “Kuna wabunge wamewekwa ndani miezi na dhamana haitoki kila siku mbunge anapelekwa mahakamani na kurudishwa tu hakuna dhamana.”

Alisema jambo hilo halipaswi kuonekana la kawaida na kutokemewa kwa sababu tu anafanyiwa mbunge wa Chadema na kudai kuwa kama wakifanikiwa kwa mbunge huyo, wanaweza kumfikia kila mmoja, “wote tutawekwa ndani.”

JPM alisema nini kuhusu Kagera?

Januari 2 mwaka huu, wakati akizungumza na wananchi katika Shule ya Sekondari Ihungo mjini Bukoba, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kutokea maafa ya tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vya watu 17, Rais Magufuli alisema Serikali haitawajengea nyumba waathirika hao na kuwataka kila mmoja abebe msalaba wake.

Akizungumzia kauli hiyo Zitto alisema: “Watu wamepoteza ndugu zao…, lakini Rais  badala ya kuwafariji anawaambia kila mmoja atabeba mzigo wake,  haya siyo maneno ya kiongozi wa serikali kuwaambia watu wake.”
  
Alisema Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya akiwa Waziri wa Fedha wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Pili, alipokuwa akiwasilisha bajeti bungeni alitamka  kuwa kutokana na hali ngumu kila mmoja aubebe mzigo wake, kauli iliyosababisha aondolewe ofisini baada ya siku tatu.

“Mnamkumbuka Mramba? (Basil-aliyekuwa Waziri wa Fedha), aliposema Watanzania watakula majani ilimradi ndege (ya rais)  inunuliwe leo yupo wapi?” alihoji

“Rais anaenda Bukoba anawaambia kuwa ni watu wa majanga tu kwamba tetemeko lao,  Ukimwi wao,  kunyauka migomba kwao, kisha  anawaambia wataubeba mzigo wao. Hii si kauli ya kiongozi.”


Mikataba ya madini

Zitto aligusia jinsi alivyoibua hoja ya ufisadi wa mgodi wa Buzwagi mwaka 2007 wakati huo kila mgodi ulikuwa ukitoa Dola 200,000 za Marekani kwa mwaka katika Halmashauri na kusababisha kuundwa kamati iliyosaidia kuzaliwa kwa sera mpya ya madini mwaka 2009 na sheria mpya ya madini mwaka 2010.

Alisema kutokana na sheria hiyo kampuni zote za madini zinalipia asilimia 0.3 ya ushuru wa huduma ya mapato ambayo kampuni inayapata.

“Leo hii Kahama mnapokea zaidi ya dola milioni 1.5m kwa mwaka. Nzega, Geita na Tarime nao wanafaidika na matunda ya kazi iliyoibuliwa na mbunge wa upinzani. Hii ndio faida ya mfumo wa vyama vingi…, nawasihi mchague diwani wa ACT hapa Isagehe ili kwenda kuongeza usimamizi wa fedha zenu katika baraza la madiwani,” alisema

Alisema licha ya kazi nzuri iliyofanyika wakati wa utawala wa Serikali iliyopita, nchi bado hainufaiki na madini kutokana na baadhi ya migodi kufungwa baada ya kampuni mbalimbali kuchimba madini na kuyamaliza.

Alisema tangu kuanza uchimbaji wa dhahabu unaofanywa na kampuni kubwa, nchi imeunza nje dhahabu zenye thamani ya Sh. trilioni 45, lakini Tanzania imeambulia Sh1.5 trilioni tu, kiwango alichodai kuwa ni kidogo kwa sababu ni chini ya asilimia nne ya mapato yote ambayo kampuni za dhahabu zimeuza katika migodi yote.

“Rais Magufuli amekuwa mkali kwa mafisadi, anatumbua watu lakini hatumsikii akitekeleza mabadiliko yaliyowekwa katika sekta ya madini ili nchi inufaike na rasirimali zake,” alisema.


Alimtaka kiongozi mkuu huyo wa nchi kuacha kutumbua watendaji aliodai kuwa ni wadogo wadogo na badala yake, ashughulike na mambo makubwa ya nchi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo