Celina Mathew
Wang Yi |
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi,
anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini Januari 9.
Mgeni huyi anatarajiwa kupokewa na mwenyeji
wake, Balozi Augustine Mahiga na kuzungumzia masuala mbalimbali likiwamo la
maboresho ya bandari ya Bagamoyo.
Aidha wakati wa ziara hiyo, Yi atakutana
pia na Rais John Magufuli kumsalimia na baadaye kufanya mazungumzo na Balozi
Mahiga kuhusu masuala ya ushirikiano wa nchi hizo mbili na wa kimataifa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji
wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga alisema madhumuni ya ziara hiyo ni
kukuza uhusiano mzuri na wa kihistoria baina ya China na Tanzania ambao upo kwa
miaka 50 sasa na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi.
"Itakumbukwa Desemba mwaka juzi
kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika na China, nchi hiyo iliichagua
Tanzania kuwa miongoni mwa nchi nne za Afrika zitakazopiga hatua ya maendeleo
ya viwanda na kupitia mpango huo, viwanda 200 vinatarajiwa kujengwa au kuwezeshwa
na China kabla ya mwaka 2020 na kuzalisha ajira kwa Watanzania 200,000," alisema.
Alisema mpango huo unakwenda sambamba na
wa Taifa wa maendeleo wa mwaka 2016-2020 na ahadi za Rais Magufuli za kujenga
Tanzania ya viwanda ambapo Watanzania wengi watanufaika kupitia ajira zitakazozalishwa.
Mindi aliongeza kuwa pia viongozi hao
wawili watazungumzia miradi mingine ya miundombinu ambapo China imeahidi
kuisaidia Tanzania kuboresha reli ya Tazara, ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na
Reli ya Kati.
Mbali ha hayo watazungumzia pia masuala
ya ushirikiano wa kimataifa ikiwa ni pamoja na mageuzi ya Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa ambapo China inaunga mkono msimamo wa Afrika na Tanzania wa
kutaka ipewe viti viwili vya kudumu kwenye Baraza hilo na kura ya turufu.
Aidha, watazungumzia amani na usalama
Afrika Mashariki na eneo la bahari ya Kusini mwa China.
Aliongeza kuwa Waziri Yi atatua na
ujumbe wa watu tisa akifuatana na waandishi wa habari wa nchi hiyo na anarajiwa kuondoka
nchini Januari 10.
0 comments:
Post a Comment