Paul Wilium,
Moshi
George Masaju |
SERIKALI
imeshindwa zaidi ya asilimia 50 ya kesi za jinai zinazofikishwa mahakamani
mkoani Kilimanjaro, kutokana na ushahidi wake kukosa nguvu.
Hali hiyo
imesababisha wapelelezi wa kesi hizo kutupiwa lawama za kukosa umakini katika kupeleleza
na kupata ushahidi.
Mwanasheria wa Serikali,
Abdallah Chavula alibainisha hayo juzi kwenye semina ya kuwajengea uwezo
iliyokutanisha maofisa wa Polisi wa wilaya zote za mkoa, Takukuru na Ofisi ya
Mwanasheria wa Serikali.
Alisema makosa
ambayo yamekuwa yakiongoza kwa kesi zao kushindwa ni ya mauaji, wizi wa kutumia
silaha na ujambazi wa kutumia silaha.
Chavula alisema
kesi hizo ushahidi wao kwa asilimia kubwa umekuwa ukiegemea kwenye utambuzi
ambao ni dhaifu na kudai kuwa mahakama hazina nguvu za kumtia hatiani
mshitakiwa, kwa kuamini ushahidi wa utambuzi peke yake.
Alisema kushindwa
kesi hizo kunatokana na ofisa upelelezi au polisi kukosa uelewa wa kanuni
na sheria ambazo hutolewa na Mahakama na jinsi ya kupeleleza.
Hivyo kutokana
na changamoto hizo askari wanatakiwa kuwa na tabia ya kujisomea vitabu vya
sheria ili kuzielewa.
Aidha, Chavula alisema
ili kuwe na upelelezi bora, askari au mpelelezi anatakiwa kuelewa sheria
na jinsi ya kupeleleza ili kufanikisha ushahidi dhidi ya makosa ya jinai.
“Jamhuri
tumekuwa tukishindwa kesi nyingi kutokana na wapelelezi mlivyotafuta ushahidi
wa kumtia mtuhumiwa hatiani, kukosa nguvu na hii inasababishwa na kutozingatia
sheria wakati wa kupeleleza, hivyo ni lazima mjijengee tabia ya kusoma vitabu
mara kwa mara, ili kutambua mnachopaswa wakati mkipeleleza,” alisema Chavula.
Alisema jukumu
la kupeleleza makosa ya jinai ni la Jeshi la Polisi na maofisa wake kwani lipo kwa mujibu wa sheria ambayo imelipa
mamlaka ya kufanya upelelezi kwa kina, ili kujenga ushahidi bila shaka yoyote dhidi
ya mtuhumiwa, ili afikishwe mahakamani na kutendewa haki.
Ofisa Mwandamizi
wa Takukuru wa Mkoa, Benedict Mongela alisema askari hawapaswi kupendelea
marafiki au jamaa zao wawapo kazini na kwamba wajibu wao ni kuzuia uhalifu kwa
haki bila upendeleo.
Mongela alisema
askari wanapaswa kuepuka zawadi haramu na kuomba au kupokea rushwa kwa mtu aliyemsaidia
au anayemhudumia, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na kimaadili ya kazi.
Aidha, Ofisa
Mwandamizi huyo wa Takukuru alibainisha kuwa mmomonyoko wa maadili umechangia ongezeko
la vitendo vya rushwa na kuitaka Polisi kushirikiana na Takukuru kupambana nayo.
0 comments:
Post a Comment