* Wakurugenzi watatu wang’olewa kisha warudishwa chuoni
* Ni siku chache baada ya Mkurugenzi Mtendaji kutumbuliwa
* Ni siku chache baada ya Mkurugenzi Mtendaji kutumbuliwa
Mwandishi Wetu
HALI si shwari ndani ya Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco). Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wakurugenzi watatu wa
shirika hilo kushushwa vyeo huku mwingine akiacha kazi.
Tukio hilo limekuja siku tano baada ya
Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo,
Felchesmi Mramba na siku moja tangu kuanza kazi kwa Dk Tito Mwinuka,
aliyeteuliwa kukaimu nafasi hiyo.
Habari za uhakika kutoka miongoni mwa
watendaji waandamizi ndani ya shirika hilo zilizolifikia gazeti hili jana, zilieleza
kuwa wakurugenzi hao watatu wamehamishiwa katika Chuo cha Tanesco (TSS)
kilichoko eneo karibu na stesheni ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Dar es
Salaam.
Uamuzi huo unaelezwa kufikiwa na Bodi ya
Wakurugenzi ya Shirika hilo chini ya uenyekiti wa Dk Alex Kyaruzi baada ya
kukutana na Dk Mwinuka na kwamba watendaji hao wameshakabidhiwa barua za
kujulishwa uamuzi huo.
Pamoja na hatua hiyo, Watson Mwakyusa
ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimaliwatu, ameamua kuacha kazi.
“Sina mengi ya kueleza kuhusu hilo. Kwa
taarifa zaidi naomba uwasiliane na Msemaji wa Tanesco kwa ajili ya ufafanuzi
zaidi,” alisema Dk Kyaruzi alipoulizwa kuhusu suala hilo.
Gazeti hili lilipomtafuta Msemaji, Leyla
Muhaji alisema hana taarifa zozote, lakini watendaji hao waandamizi
walilithibitishia gazeti hili kuwa watendaji hao wameshushwa vyeo.
Walioshushwa vyeo ni Naibu Mkurugenzi wa
Uwekezaji wa Shirika hilo, Decklan Mhaiki, aliyekuwa Mkurugenzi wa Usambazaji,
Sophia Mgonja na Johary Kachwamba aliyekuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji.
Mramba uteuzi wake ulitenguliwa Januari
mosi na Rais Magufuli ambaye papo hapo alimteua Dk Mwinuka ambaye ni msomi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Uamuzi huo ambao haukuelezwa sababu,
ulichukuliwa muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuwaweka kikaangoni vigogo
waliotangaza kupandisha bei ya umeme, akisema hatua hiyo ni ushahidi kuwa bado
kuna ‘majipu’ na ataendelea ‘kuyatumbua’.
Sakata hilo liliibuka baada ya Desemba
30 mwaka jana, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura)
kukubali maombi ya Tanesco ya kupanda kwa bei ya umeme kuanzia Januari mosi kwa
asilimia 8.5.
Hatua hiyo ilizuiwa na Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo huku Rais Magufuli akisema hatua hiyo
ilikuwa inakwamisha mipango ya Serikali inayojiandaa kuelekea katika uchumi wa
viwanda.
Ewura katika agizo lake namba 16-126,
inaruhusu Tanesco kupandisha bei ya umeme kwa kiwango hicho, sambamba na
kutekeleza maagizo zaidi ya 10, ikiwamo kuzalisha umeme kwa mitambo yenye
gharama nafuu.
Uamuzi wa Ewura kuridhia maombi ya
Tanesco uliwachanganya wananchi kutokana na kauli iliyotolewa mwaka juzi na
Profesa Muhongo kuwa kazi yake kubwa ni kuhakikisha bei ya umeme inashuka, huku
wakishuhudia Aprili mwaka jana Tanesco ikishusha bei ya umeme kwa kati ya
asilimia 1.5 na 2.4.
Hata hivyo, Oktoba mwaka jana, Tanesco
iliwasilisha maombi mapya ya kutangaza ongezeko la bei kwa maelezo kwamba
wamekuwa wakipata hasara ya Sh bilioni 40 kila mwezi, maombi ambayo Desemba 31
mwaka jana yalipingwa na Profesa Muhongo, kisha Januari mosi kuwekewa msisitizo
na Rais Magufuli.
“Tupo katika majonzi makubwa na mshituko
baada ya kuwepo kwa taarifa hizo,” alisema mmoja wa watumishi wa Shirika hilo.
0 comments:
Post a Comment