Salha Mohamed
Mohamed Mpinga |
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama
Barabarani, limeanza operesheni ya kukamata magari yenye taa zenye mwanga mkali
‘spot light’.
Operesheni hiyo itakayokuwa endelevu
itahusisha magari yaliyoongezwa taa za ziada kwa kile kinachodaiwa kuwa ni
urembo kwenye magari.
Uwekaji wa taa hizo ni kinyume cha
sheria ya usalama barabarani kifungu cha 39 sura ya 168 kama ilivyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani
nchini, Mohamed Mpinga, alisema jana kwamba utekelezaji wa operesheni hiyo unatokana
na katazo alilitoa Desemba 22 mwaka jana.
“Nilisema kuwa hivi karibuni kumezuka
mtindo wa kuweka taa zinazotoa mwanga mkali hasa kwenye vyombo vya moto kuanzia
pikipiki hadi magari makubwa,” alisema.
Alisema taa hizo zimekuwa kero kwa
madereva wengine na kusababisha ajali, hivyo aliwataka wamiliki wa magari
kuzitoa kabla hawajayakamata.
Mpinga alisema madereva watakaokamatwa
watachukuliwa hatua za kisheria, kwani tayari maelekezo yametolewa nchi nzima.
“Nimeshatoa maelekezo nchi nzima, kwamba
kwa watakaokuwa wameweka taa kwenye magari makubwa, wengine huweka nyingi na
kusababisha matatizo, kwani mwanga mkali hufanya dereva mwingine aache barabara
na kusababisha ajali,” alisema.
Alifafanua kuwa wapo madereva
wakimulikwa hupofuka kwa muda mfupi jambo linaloweza kusababisha ajali.
“Kama taarifa tulitoa muda wa kutosha
tangu Decemba 22 hadi leo (jana) ni siku za kutosha kwa kutoa hadhari kwa
wananchi,” alisema.
Alisema operesheni hiyo haitahusisha
magari yaliyokuja na taa maalumu kutoka kiwandani pamoja na ya uwindaji.
“Kuna magari mengine huweka kwa sababu
yanatumika kwa uwindaji, hayatahusika ila yanapoingia barabarani wanatakiwa
kuzifunika
“Kuna mtindo wa magari makubwa kuweka
taa kubwa nyuma zikimulika, mtu anayemfuata anaweza kufikiri gari linakuja
kumbe linakwenda mbele,” alisema Mpinga.
0 comments:
Post a Comment