Mwandishi Wetu
Samia Suluhu |
TANZANIA
imechaguliwa kuwa miongoni mwa nchi saba zilizoingizwa katika Mpango wa Ukanda
wa Kimkakati wa Kiuchumi wa China.
Mpango
huo ulibuniwa na Serikali ya China kwa dhamira ya kukutanisha jumuiya za wafanyabiashara
za Mashariki mwa Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika, kubadilishana mawazo
kuhusu kuwezesha biashara kuchangia kwenye uchumi wa mataifa yao.
Nchi zingine
zilizochaguliwa kuingizwa kwenye mpango huo ni Malaysia, Sri Lanka, Nepal,
Bangladesh, Pakistan na Thailand.
Taarifa
ya Ofisi ya Makamu wa Rais iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa
nafasi hiyo ya Tanzania, imepatikana baada ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan kufanya mazungumzo na mfanyabiashara wa madini na vito kutoka China, Dk
Hellen Lau.
Makamu
wa Rais, ambaye pia ni mjumbe wa jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN),
la kumwezesha mwanamke kiuchumi, akiwakilisha nchi za Ukanda wa Kusini na
Mashariki mwa Afrika, alikutana na Dk Hellen Septemba mwaka jana kwenye mkutano
wa Guangdong, China.
Taarifa
hiyo ilieleza kuwa katika mkutano huo, Makamu wa Rais alimwomba Dk Hellen aisaidie
Tanzania kuwasilisha maombi ya kuwa kwenye mpango huo na yalikubaliwa na kupata
uanachama kwenye mpango huo mkubwa maarufu kama ‘China One Belt, One Road’.
Kutokana
na uteuzi huo, Makamu wa Rais alikutana na watendaji wa Taasisi ya Sekta
Binafsi Tanzania (TPSF), Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Biashara
(TCCIA) na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), kuwaeleza kuhusu muhimu wa
Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo.
Taarifa
hiyo ilieleza kuwa Samia alisema kwenye mpango huo kila nchi mwanachama imepewa
ofisi kwenye jengo la 21st Century Maritime Silk Road Expo, bila
kulipia kwa miaka mitatu, ili ioneshe na kutangaza bidhaa zake.
Samia aliwaagiza
watendaji wa sekta binafsi wajipange na kuweka mikakati ya namna ya kunufaika
na mpango huo haraka iwezekanavyo.
Alisema
Tanzania pia itanufaika na fedha za mfuko kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu,
ambazo zinatolewa kwa nchi zilizojiunga na mpango huo.
Mwenyekiti
wa TPSF, Godfrey Simbeye na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye
Viwanda na Wakulima Zanzibar, Taufik Turki walimwahidi Makamu wa Rais kutumia
fursa hiyo ipasavyo kukuza biashara kati ya Tanzania na wanachama wa mpango
huo.
0 comments:
Post a Comment