Jemah Makamba
WALINZI wa kampuni ya SGA wamefikishwa kwenye
Mahakama ya Wilaya ya Ilala wakituhumiwa kula njama, kuvunja na kuiba ya vitu
venye thamani ya Sh milioni 197 mali ya kampuni ya TATA Holdings Tanzania Ltd.
Watuhumiwa hao ni Godfrey Gosbert (23),
James Edward (26), Ubaya Simba (33), Michael Moses (26), Musa Mukaubani (22) na
Halfan Mohamed (35).
Akisoma mashitaka hayo jana mbele ya
Hakimu Adelf Sachore, mwendesha mashitaka Florida Wenceslaus alidai kuwa Desemba
mwaka jana washitakiwa walikula njama kwa nia ya kuiba.
Ilidaiwa pia Mahakamani hapo kuwa Desemba
13 mwaka jana, washitakiwa wakilinda ghala la kampuni hiyo, walivunja kwa nia
ya kuiba.
Katika hatua nyingine, ilidaiwa kuwa
Desemba 13 usiku walivunja na kuiba vitu mbalimbali zikiwamo zana za kilimo na
mbolea zote zikiwa na thamani ya Sh milioni 197.
Hata hivyo, mwendesha mashitaka alidai kuwa
washitakiwa wote kwa pamoja walishitakiwa kwa kosa lingine la kushindwa kuzuia
uhalifu dhidi ya Kampuni hiyo iliyopo barabara ya Nyerere wakiwa kama walinzi.
"Sina kipingamizi na dhamana kama
washitakiwa watakidhi masharti kwani kosa lao linadhaminika," alisema
Wenceslaus.
Hakimu alisoma masharti ya dhamana ikiwa
ni wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi inayofahamika na mmoja awasilishe
hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 32 na kusaini ahadi ya Sh
milioni 32.9.
Washitakiwa waliita wadhamini wao lakini
hakuna aliyekidhi masharti ya dhamana hakimu akasema kesi hiyo itatajwa Januari
16, washitakiwa wote wakarudishwa rumande.
0 comments:
Post a Comment