Celina Mathew
Ben Saanane |
SAKATA la aliyekuwa Msaidizi wa
Mwenyekiti wa Chadema, Ben Saanane, limeendelea kuwa kitendawili baada ya
kuelezwa kuwa hadi sasa hakuna taarifa zozote kuhusu kupotea kwake.
Hatua hiyo inatokana na takribani miezi
miwili kukamilika tangu kupotea kwake na hadi sasa hajulikani aliko huku
uchunguzi ukiendelea kufanywa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam likishirikiana
na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Akizungumza na JAMBO LEO jana, Msemaji
wa Chadema, Tumaini Makene alisema mambo matatu yaliyosemwa na Chadema endapo
yatatimizwa basi itajulikana Saanane aliko.
Alitaja mambo hayo kuwa ni pamoja na
Serikali kueleza mahali aliko, kwa kuwa ina jukumu la kulinda raia licha ya
kwamba Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna wa Polisi,
Robert Boaz, kueleza kuwa suala hilo linafuatiliwa.
Aliongeza kuwa mamlaka husika za
mawasiliano zinapaswa zieleze kwa mara ya mwisho alifanya mawasiliano lini,
wapi na nani, maana ndio wenye uwezo wa kuamuru mashirika ya mawasiliano
kusema.
Hata hivyo, JAMBO LEO lilipomtafuta Kamanda
wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro ili kutolea ufafanuzi
suala hilo, aliomba atafutwe saa 11 jioni kwa kuwa alikuwa mkutanoni.
"Kwa sasa nipo mkutanoni, naomba
nitafutwe kuanzia saa 11 jioni, ndio nitakuwa nimemaliza na nitakueleza kuhusu
suala hilo," alisema Sirro.
Katika mkutano na waandshi wa habari
hivi karibuni, Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu alisema kabla ya
Saanane kupotea, aliandika katika mitandao ya kijamii akihoji uhalali wa
Shahada ya tatu ya Rais John Magufuli na kupokea vitisho vingi.
Alisema hatua hiyo ilikuja baada ya Rais
kuanzisha mchakato wa uhakiki wa vyeti kwa watumishi mbalimbali ambapo yeye
aliliendeleza kwenye mitandao ya kijamii.
“Hii ni muhimu kwa kuwa katika miezi sita,
watu wengine wanakamatwa kwa kuandika vibaya kuhusu Rais kwenye mitandao, mimi
nilisema dikteta uchwara nikadhibitiwa kesho yake, kuna watu 140 walikamatwa
kwa kumkosoa hivyo hata suala hilo linaweza kuwa mojawapo,” alisema Lissu
kwenye mkutano huo.
0 comments:
Post a Comment