*Adai ‘umebaka’ mpaka mfuko wake, ashindia uji
*Amwambia mwanawe
hicho ni kipimo cha imani
Leonce Zimbandu
WIKI moja baada ya Rais John Magufuli kusema fedha
zitapotea mpaka makanisani, Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG)
Viwege, Fulgency Bunduki amesimulia ukata ulioingia kanisani akisema ‘umebaka’
mfuko wake.
Jumapili ya kwanza ya mwaka huu, Rais Magufuli akiwa kwenye
Kanisa la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma wilayani Bukoba mkoani Kagera,
aliwataka viongozi wa dini wamvumilie, kwa kuwa fedha zitaendelea kupotea hata kwenye
nyumba hizo za ibada.
Rais Magufuli alisema zamani kulikuwa na fedha za hovyo
hovyo, lakini sasa anachotaka ni kila mtu aendelee kula anachostahili, huku
akiwataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii kama maandiko matakatifu
yanavyoelekeza kuwa asiyefanya kazi na asile, badala ya kulalamika kuwa fedha
zimepotea.
Kwa kawaida vyanzo vikuu vya mapato kwenye nyumba hizo za
ibada kwa maana ya makanisa na misikiti huwa ni sadaka zitolewazo na waumini.
Ukata
Akizungumza juzi kwenye ibada ya kuaga mwili wa mjumbe wa
shina la CCM la Majengo Mapya, Kwa Mhaya, Kivule wilayani Ilala, Dar es Salaam,
Mchungaji Bunduki alisema maisha yamekuwa ‘pasua kichwa’ si kwa wananchi pekee,
bali hata kwa wachungaji, akiwamo yeye ambaye mfuko wake ‘umebakwa’ na ukata.
Akielezea visa vinavyoambatana na ukata, Mchungaji Bunduki
alitoa mfano wa mwaka jana, siku aliyolazimika kunywa uji na familia yake mchana,
ambapo mtoto wake wa kike aliuliza sababu za kunywa uji mchana na kuhoji kama
baba yake ‘amefulia (amefilisika)’.
“Nilimjibu kuwa si kufulia bali njaa imebaka hata mifuko
yangu, hivyo tuvumilie Mungu atatusaidia kusonga mbele,” alisema huku mamia ya
waombelezaji wakivunja mbavu kwa kicheko.
Imani
Mchungaji Bunduki alisema kwa hakika hakuna binadamu
aliyezaliwa na mwanamke atakayekwepa kifo, hivyo vikwazo vinavyotokea kwenye
maisha sasa, ni matokeo ya kujiimarisha kiimani.
Alisema kutokana na hali mbaya ya maisha, baadhi ya Wakristo
na Waislamu wamekuwa wakitoa visingizio vya kubanwa na kazi, kiasi cha kukosa muda
wa kuhudhuria ibada makanisani au misikitini.
“Hii ni hatari mpaka kifo kinapotokea ndipo wachungaji au
maimamu waonekane bora? Bora kusimamia usemi unaosema heri kuswali kabla
hujaswaliwa,” aliwaasa waombolezaji.
Kukimbiwa
Baada ya Mchungaji Bunduki kumaliza kutoa mahubiri hayo,
Mchungaji mwenyeji wa Kanisa hilo, Charles Mazengo aliasa waumini wa dini zote
kuendelea kumwomba Mungu kwenye nyumba za ibada.
Alisema watu wamekuwa wasanii, kwani wanapoulizwa kuhusu
Kanisa wanaloabudu, wamekuwa wakielekeza kwa vidole “ni pale”, lakini hata siku
moja hawajawahi kufika kwenye Kanisa husika.
Mwenyeki wa Serikali ya Mtaa, Thomas Nyanduli aliwataka
wakazi wa Majengo Mapya kuanzisha Mfuko wa Kufa na Kuzikana kwa vile hakuna
ajuaye siku yake.
“Leo tumekusanyika hapa na kushikana mashati kwa ajili ya
michango, lakini kama Mfuko ungekuwapo nguvu isingetumika, hivyo ni busara
kujiwekea akiba,” alisema.
Uchunguzi wa gazeti hili kwa waumini wa makanisa mbalimbali,
umeonesha kuwa baadhi ya yameanza kukusanya sadaka pungufu siku za ibada,
ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita.
Muumini wa moja ya makanisa ya Kimara, alilieleza gazeti
hili kuwa kila wiki kwenye Kanisa analoabudu, walikuwa wakisomewa sadaka za hadi
Sh milioni 20, lakini sasa kufikisha jumla kuu ya Sh milioni 10 ni nadra.
Mwingine wa Kanisa lililoko Hananasif, alidai kuwa Desemba
mwaka jana kulijitokeza dalili za kupungua kwa sadaka na waumini, ingawa hakuwa
na uhakika kama hali hiyo ilitokana na ukata unaozungumzwa.
0 comments:
Post a Comment