Sharifa Marira, Rufiji
Mohamed Mchengerwa |
MBUNGE
wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM), amesema viongozi wengi serikalini ni
wafugaji ndiyo maana wanashindwa kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji,
ambayo imekuwa ikisababisha madhara makubwa kwa wananchi.
Mchengerwa
alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Mgomba Kati,
walioeleza jinsi wafugaji wanavyoingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wananchi,
wakiwa hawajavuna.
"Wafugaji
wanatuumiza, lakini haya yote ni kwa sababu viongozi wengi ni wafugaji, hivyo
wanashindwa kuingilia kati suala hili, badala yake wanaacha wananchi wauane
kila kukicha, utafika wakati tutashindwa kuvumilia haya, tunakufa njaa na
umasikini kwa sababu ya watu.
"Yametokea
matukio makubwa ya kuuawa wananchi wawili kwenye kijiji cha Kilimani mwezi jana,
lakini sikuona kiongozi wa Serikali aliyetoa tamko au hata kufika eneo la tukio,
vivyo hivyo hata kwa yule mwananchi wa Morogoro aliyechomwa mkuki kinywani
ukatokea shingoni, viongozi wametulia tu," alisema.
Alisema
si Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, Naibu wake, William ole
Nasha wala makatibu wakuu wao, waliofika maeneo yaliyoathirika au hata kutolea makatazo dhidi ya mambo hayo na kwamba ndiyo
matunda ya viongozi wengi wafugaji hivyo kushindwa kutafuta suluhisho la
kudumu.
Alisema
kuwapo mifugo Rufiji kulitokana na rushwa ya viongozi waliokuwa madarakani
miaka ya 2005, ambao walitoa mifugo kwenye bonde moja ili lisiharibike na
kupeleka bonde lingine ili kuua wananchi
wa maeneo hayo.
"Mifugo
hapa kwetu ilikuja mwaka 2005, ilihamishwa kutoka bonde la Ihefu, Iringa, kwa
kuwa lilikuwa likiharibika, lakini cha kushangaza ikaletwa bonde la Rufiji ili
liharibike nasi wananchi tupate shida na ndicho kinachotokea leo hii," alisema
Mchengerwa.
Alieleza
kuwa alichaguliwa na wananchi kuwawakilisha vema na kutetea maslahi yao na
ndicho anachokifanya na hatarudi nyuma katika kudai haki na maendeleo ya Rufiji, kwani
imekuwa nyuma kwa miaka mingi kutokana na kukosa wawakilishi wenye nia ya dhati
ya kuwasaidia.
0 comments:
Post a Comment