Celina Mathew
WASICHANA wa kazi wametajwa kuwa chanzo cha kuvurugika
kwa ndoa nyingi Dar es Salaam, kutokana na uhusiano zaidi ya kazi za nyumbani
wanaokuwa nao na mabosi wao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika mahojiano
maalumu jana, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Dawati la Jinsia wa Wilaya
ya Kinondoni, Inspekta Prisca Komba alisema visa vya wasichana hao vimekuwa
vikiripotiwa Polisi.
Inspekta Prisca alisema kwa upande wa mabosi wa kiume,
wasichana hao wamekuwa wakishirikiana nao ngono mara nyingi baada ya mabosi
kutumia kilevi, lakini wakati mwingine wakibakwa.
"Unakuta baba anakunywa pombe na kulewa sana na
anaporudi nyumbani kama mama hayupo, anaamua ‘kutembea’ na mfanyakazi wake wa
ndani, jambo linalofanya kina mama kuja kushitaki kwa kuwa baada ya hapo wengine
hufukuza wake zao na kuwapiga wanapowahoji," alisema.
Kwa upande wa wanaume, Inspekta Prisca alisema baadhi
wamekuwa wakilalamika kuwa wasichana wa kazi wamegeuka makuwadi wa wake zao, jambo
wanaloona kuwa wananyanyasika.
Alitoa mfano wa mwaka jana, ambao wanaume 25 walifungua
kesi za kudhalilishwa na wake zao kwa kunyimwa unyumba hali iliyowasababishia
kuchepuka.
"Unakuta mwanamke anamwambia mumewe kwamba ana maumbile
madogo wakati walishazaa watoto wawili na kuna baadhi ya wanawake
walilalamikiwa kuhodhi mali za waume zao na kuzipeleka kwa ndugu zao ambao
hawahusiki nazo," alisema.
Alisema wanawake watano walihodhi mali na wengine wawili
walilalamikiwa kuwa na nyumba ndogo.
Akizungumza kisa asichokisahau katika Dawati hilo, Inspekta
Prisca alisema ni cha binti Yusta Lucas (20), mwenyeji wa Tabora ambaye alifika
Dar es Salaam kufanya kazi za ndani na kufanyiwa ukatili wa kung’atwa meno na bosi
wake.
Alisema kesi ya binti huyo ilimalizika Novemba mwaka jana,
ambapo mhusika alihukumiwa kifungo cha maaka miwili na faini ya Sh milioni 2 na
kufungwa kifungo cha nje.
Kwa mujibu wa Inspekta Prisca, asilimia tano ya wanawake
wamekuwa wakilalamika kunyimwa unyumba na waume zao, jambo linalowafanya kutoka
nje ya ndoa na baadhi ya wanaume pia hukataliwa na wake zao.
Alisema kwa kiasi kikubwa, hali hiyo husababishwa na
kukua na kubadilika kwa sayansi na teknolojia, ambayo baadhi yao wamekuwa
wakijidanganya nayo.
Wakwe
Inspekta Prisca alisema kunapokuwa na kesi za visa vya
mama wakwe na mawifi, wamekuwa wakiwaita wakwe na kuwaeleza kuwa wao
walishafanikiwa kwenye ndoa zao zilizodumu, hivyo wawaache watoto wao nao
wafaidi ndoa zao badala ya kuziingilia.
"Wapo kinamama wengi wanaopigania sana watoto wao wa
kike walioolewa hadi ndoa zao zinakosa nguvu,” alisema.
Alitaja pia changamoto ya wanaume walioacha wake zao kuamua
kubaki na watoto, ili wanyanyase watalaka wao, wakati sheria inasema kila mtoto
anatakiwa kukaa siku 15 kwa mama na nyingine 15 kwa baba.
Akizungumzia takwimu za mwaka jana kuanzia Januari hadi
Desemba, Inspekta Komba alisema kesi zilizoripotiwa za kubaka zilikuwa 62,
kulawiti 19, shambulio la aibu 12, kutorosha watoto 23 na kutelekeza familia 32.
Kesi 12 za kufanya mapenzi na wanafunzi ziliripotiwa,
kuwapa mimba wanafunzi 13, shambulio la kimwili 33, kujeruhi tisa, ukatili wa
watoto moja, kutorosha wanafunzi 12, kunajisi moja na kujaribu kubaka tatu.
0 comments:
Post a Comment