Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ,amemwagiza
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhakikisha eneo la
Kisarawe II linapata umeme wa uhakika ili kuwezesha viwanda na wananchi wa eneo
hilo kuzalisha.
Alitoa agizo hilo jana alipotembelea
kiwanda cha Milkcom kinachozalisha bidhaa za maziwa na cha Watercom
kinachozalisha maji katika kata ya Kisarawe II Kigamboni, akiwa kwenye ziara ya
kikazi.
“Waziri wa Nishati ahakikishe eneo hili
linapata umeme wa uhakika, ili kuwezesha viwanda hivi kufanyakazi vizuri jambo
litakaloongeza uzalishaji. Pia wananchi wanaoishi maeneo haya nao watanufaika
na upatikanaji wa nishati hiyo,” alisema.
Waziri Mkuu alisema amefarijika na
jitihada za mwekezaji huyo za kuunga mkono mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano
wa kuifanya Tanzania kujenga uchumi wa viwanda utakaowezesha Taifa kufikia
uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Awali, Msemaji wa Viwanda hivyo,
Aboubakar Faraj katika taarifa ya viwanda hivyo kwa Waziri Mkuu, alisema moja
ya changamoto zinazowakabili ni upatikanaji wa umeme wa uhakika jambo linalosababisha
kupanda kwa gharama za uzalishaji.
“Umeme unapokatika tunalazimika kutumia jenereta
kwa muda mrefu. Hii husababisha ongezeko la gharama za uzalishaji ambazo
huumiza kiwanda kwa sababu haiwezekani kumtwisha mzigo huu mlaji,” alisema.
Faraji alisema changamoto nyingine ni
miundombinu ya barabara, ambayo husababisha wateja wengi kushindwa kufika
kwenye viwanda hivyo kirahisi, hivyo aliiomba Serikali kuwatatulia kero hiyo.
Aliongeza kuwa kwa sasa viwanda hivyo
vimeajiri watu zaidi ya 1,800, ambapo alisema endapo Serikali itawahakikishia
upatikanaji wa umeme na barabara wataongeza ajira kwa asilimia 25 mwakani.
Mapema Waziri Mkuu alizindua wodi ya
wazazi kwenye zahanati ya Kisarawe II iliyojengwa kwa ufadhili wa kampuni ya
mafuta ya Oilcom. Wodi hiyo yenye vyumba vitatu itawapunguzia akina mama
kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
0 comments:
Post a Comment