Grace Gurisha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshindwa
kutoa uamuzi wa ama kufuta mashitaka ya mauaji dhidi ya mke wa marehemu
bilionea Erasto Msuya, Miriam Msuya (41) au la, anayetuhumiwa kumwua dada wa
marehemu, Aneth kutokana na wakili wa washitakiwa hao, Peter Kibatala kutokuwapo.
Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa wa Mahakama hiyo alisema
jana kuwa hawezi kusoma uamuzi huo, kwa sababu Kibatala hayupo ana dharura na
pia ni vizuri yeye mwenyewe akawepo kutokana na kwamba ndiye alitoa hoja ya kutaka
kufutwa kwa mashitaka hayo.
Kutokana na hali hiyo, Mwambapa aliahirisha kesi hiyo
hadi Januari 9 kwa uamuzi. Awali, uamuzi huo ulitakiwa kutolewa Agosti 10,
lakini kila ilipofika tarehe ya uamuzi ziliibuka sababu tofauti tofauti na kesi
kuahirishwa.
Hatua hiyo ilifikiwa na Mahakama hiyo ya kutoa uamuzi, baada
ya Wakili wa Miriam, Kibatala kuwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi
Magreth Bankika wa Mahakama hiyo kuwa hati ya mashitaka ina kasoro na kuomba
ifutwe huku akidai kuwa wateja wake waliteswa na polisi.
Mbali na Miriam, mshitakiwa mwingine kwenye kesi hiyo ni
mfanyabiashara wa Arusha, Revocatus Muyela (40), ambapo Kibatala alidai pia
kuwa washitakiwa hao waliteswa na askari kabla ya kuchukuliwa maelezo ili
wakiri kuhusika na mauaji hayo.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Diana Lukondo alisema
hati ya mashitaka iliyokuwa mahakamani iko sahihi kwa kuwa ina sababu zote za
kuitwa hati ya mashitaka, kwa hiyo hoja za Kibatala hazina mashiko.
Muyela aliunganishwa kwenye kesi hiyo, baada ya kukamatwa
na kubainika kutuhumiwa kwenye mauaji hayo. Aneth alikuwa dada wa marehemu Msuya
na alichinjwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Dar es
Salaam Mei 26 mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment