Celina Mathew
David Kafulila |
ALIYEKUWA Mbunge wa Kigoma Kusini, David
Kafulila, amesema atapokelea kadi ya Chadema jimboni mwake baadaye mwezi huu.
Kafulila alitangaza kuhama NCCR-Mageuzi
na kurudi Chadema kwa alichoeleza kuwa ndicho chama kilichojipambanua kuelekea
safari ya mabadiliko ifikapo mwaka 2020.
Kada huyo tayari amewasilisha barua kwa
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe kumjulisha kuwa anajivua uanachama
na anarudi Chadema.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi
jana, Kafulila alisema ameamua kuwa atapokelea kadi hiyo jimboni kutokana na
mapenzi aliyonayo kwa wananchi wake.
"Nimepanga kuchukua kadi mwezi huu
jimboni, kwa kuwa ilikuwa nichukue kadi mwanzoni lakini ilishindikana kutokana
na siku kuu, hivyo siku yoyote kuanzia sasa nitachukua," alisema.
Wakati anajiuzulu NCCR-Mageuzi na kurudi
Chadema, alisema hakufanya uamuzi kwa kukurupuka bali alitafakari na kushauriwa
na wananchi wa jimbo lake, na kuridhika kurudi huko.
"Nilitafakari na kushauriwa sana
jimboni na kuridhika kwamba Chadema ndiko sehemu inayojipambanua kwa mikakati
ya kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania na ni vema kukusanya nguvu ya
kila mwenye kiu ya mabadiliko ndani ya chama kimoja, ili kufupisha safari ya
mabadiliko," alisema.
Alipoulizwa kwa nini amerudi Chadema wakati
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk
Wilbrod Slaa alipata kumwita sisimizi kwa alichoeleza kuwa hakuwa na imani naye, alijibu
kuwa siasa ni malengo si uhusiano binafsi.
Kafulila aliongeza kuwa wanasiasa wanaunganishwa
na malengo zaidi ya urafiki na kwamba malengo yake sasa ni kuendelea kupigania
mabadiliko ya kimfumo yanayoenea zaidi kwenye chama hicho (Chadema) kuliko
kingine.
Novemba 10, 2009 Kafulila alijivua
uanachama wa Chadema na kuhamia NCCR-Mageuzi kutokana na kuondolewa kwenye
nafasi ya uofisa habari wa chama hicho.
Pia akiwa NCCR-Mageuzi, alitimuliwa
uanachama kwa kudaiwa kukiuka taratibu za chama hicho na tuhuma za kutaka
'kumpindua' Mwenyekiti, James Mbatia.
Hata hivyo, suala hilo lilipata suluhu
baada ya Mbatia kuteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Mbunge. Wakiwa
bungeni, Mbatia na Kafulila walikutana, kuzungumza na hatimaye kumaliza mzozo wao.
0 comments:
Post a Comment