Mwandishi Wetu
WIZARA ya Nishati na Madini kwa
kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira ya Zanzibar,
zinatarajia kuunda Kamati maalumu kwa ajili ya
kuandaa mpango wa ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika sekta za gesi na mafuta.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo alibainisha hayo katika
kikao chake na Waziri wa Ardhi, Maji,
Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib
aliyeambatana na ujumbe wake.
Kikao
hicho kilihudhuriwa na watendaji kutoka
Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Wakala
wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA)
na Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (PURA).
Profesa Muhongo alisema lengo la kamati
hiyo ni kujadili maeneo ya kushirikiana pamoja na kubadilishana uzoefu katika sekta
za gesi na mafuta.
Alisema kamati hiyo itashirikisha wataalamu
kutoka katika taasisi za Sheria, ardhi, kodi, gesi na mafuta chini ya makatibu wakuu wa sekta husika
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Waziri Muhongo alisema uwepo wa kamati hiyo
utachochea Zanzibar kuwa na taasisi kama TPDC na nyingine, hivyo kupelekea
ukuaji wa sekta ya gesi na mafuta.
Alisisitiza kwamba Serikali ya Tanzania Bara kupitia Wizara ya Nishati na Madini ipo tayari
kushirikiana na Serikali ya Zanzibar pamoja na kubadilishana uzoefu
katika masuala ya gesi na mafuta.
Profesa Muhongo alishauri Serikali ya
Zanzibar kuandaa wataalam wa mafuta
na gesi kwa kuwasomesha katika
ngazi za diploma na shahada katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Madini Dodoma (MRI).
Akiongeza Serikali ipo tayari kutoa ufadhili
kwa wanafunzi wa Zanzibar wanaofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kwa ajili ya kusomea shahada ya
uzamili katika vyuo vya ndani na nje ya nchi.
Naye Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na
Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib, alimshukuru Waziri Muhongo kwa utayari
wa Wizara ya Nishati na Madini katika kushirikiana na Wizara yake kwenye
shughuli za mafuta na gesi
Alisema kamati itakayoundwa itapelekea
mambo kwenda kwa kasi na kuwa na data za pamoja zinazotokana na utafiti wa mafuta
na gesi na kupanga Mikakati ya kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.
0 comments:
Post a Comment