Grace Gurisha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,Dar es Salaam imetoa siku
mbili kwa upande wa Jamhuri kubadilisha hati ya mashitaka ya mauaji dhidi ya mke wa bilionea Erasto
Msuya (marehemu), Miriam Msuya (41), anayetuhumiwa kumwua dada wa Msuya, Aneth,
baada ya kubainika kuwa hati hiyo ina kasoro.
Pia Mahakama hiyo imeitaka mamlaka husika itoe fomu ya
matibabu (PF3) kwa Miriamu na mshitakiwa mwingine, Revocatus Muyela (40)
wakatibiwe, baada ya kuieleza Mahakama kuwa waliteswa na polisi ili wakiri
kutenda kosa hilo.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Godfrey
Mwambapa wa Mahakama hiyo, akisema baada ya kupitia hati hiyo, alibaini kasoro
mbili za kisheria, kuwa hati hiyo haioneshi mtu mmoja kusababisha kifo cha mtu
mmoja.
Kasoro ya pili, Mwambapa alisema mtu aliyesababisha kifo
haonekani kama ana nia ovu, kwa hiyo washitakiwa hawaonekani kama walitenda
kosa hilo, hivyo Mahakama inaona hati hiyo ni mbovu na si sahihi.
“Siwezi kusema hati hii ni sahihi kwa sababu tu imepokewa
na Mahakama, kwa hiyo kasoro hii inatakiwa irekebishwe ndani ya siku mbili.
Hatua hiyo inatokana na Mahakama kuwa na mamlaka ya kusahihisha hati ya mashitaka
kabla ya kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na pia inaweza kuamuru hati
ibadilishwe,” alisema Mwambapa
Katika suala la kuteswa kwa washitakiwa, Hakimu Mwambapa
alisema Mahakama inaona suala hilo ni la msingi, hivyo hatua za makusudi
zinaweza kuchukuliwa yanapotokea malalamiko kama hayo, hivyo alikubaliana na
hoja za wakili wa utetezi Peter Kibatala, kuwa Mahakama haizuiwi kuamuru
mamlaka husika kuwapa PF3.
Alisema hatua hiyo inatokana na kwamba Mahakama haina
utaalamu kuhusu masuala ya kiafya, kwa hiyo yanapotokea lazima yafikishwe kwenye
mamlaka husika hivyo inatakiwa iwape fomu ili wakapewe matibabu, lakini haina
maana Mahakama inahitaji matokeo hayo.
Alisema hati ibadilishwe na ipelekwe mahakamani na kesi
iliahirishwa hadi Januari 11 Jamhuri itakapokuwa imerekebisha kasoro zilizopo.
Hatua hiyo ilifikiwa na Mahakama hiyo, baada ya Kibatala
kuwasilisha maombi hayo kwa Hakimu Mkazi Magreth Bankika kuwa hati ya mashitaka
ina kasoro na kuomba ifutwe pia akidai kuwa wateja wake waliteswa na polisi.
Mbali na Miriam, mshitakiwa mwingine ni mfanyabiashara wa
Arusha, Revocatus Muyela (40), ambapo Kibatala alidai pia kuwa washitakiwa hao
waliteswa na askari kabla ya kuchukuliwa maelezo ili wakiri kuhusika na mauaji
hayo.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Diana Lukondo alidai
kuwa hati hiyo ya mashitaka iko sahihi kwa kuwa ina sababu zote za kuitwa hati
ya mashitaka, hivyo hoja za Kibatala hazina mashiko.
0 comments:
Post a Comment