Celina Mathew
Zitto Kabwe |
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT),
ameitaka Serikali kuzungumza na Kenya haraka ili Watanzania wanaouza gesi ya
kupikia nchini humo waendelee kutumia bandari ya Dar es Salaam.
Kauli ya Zitto imetokana na hatua ya Wizara
ya Nishati ya Kenya, kupiga marufuku gesi ya kupikia kutoka Tanzania ndani ya
siku saba.
Zitto alisema tamko lilitolewa na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Kenya lilisema kuwa ndani ya siku saba kuanzia
Aprili 24 itakuwa ni marufuku Kenya kuagiza gesi ya kupikia kutoka Tanzania.
“Uamuzi huu wa Kenya ni kinyume na
misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambamo Tanzania na Kenya ni wanachama.
Kwa mujibu wa Itifaki ya Soko la Pamoja, bidhaa za nchi zetu zinaruhusiwa
kusambaa ndani ya Jumuiya bila vikwazo,” alisema.
Alisema gesi ya kupikia kuingia Kenya
hutoka nchini, kwa sababu Tanzania ndiyo pekee katika ukanda huu ambayo
imewekeza mitambo ya kupokea gesi na kuisindika mitungini katika bandari ya Dar
es Salaam na mfumo mzuri zaidi wa kupokea gesi kuliko bandari ya Mombasa, hivyo
kuifanya gesi ya nchini kuwa na gharama nafuu Kenya kuliko inayopitia Mombasa.
Aliongeza kuwa uamuzi wa kuzuia gesi ya
Tanzania unalenga kulinda bandari ya Mombasa kwa kuvunja mkataba wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kutaka kuifanya Tanzania iendelee kuwa muuzaji wa malighafi
kwenda Kenya badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani kama gesi ya kupikia.
“Uamuzi huu wa Serikali ya Kenya una
lengo la kuathiri urari wa biashara kati yake na Tanzania ambapo kwa miaka ya
karibuni, Tanzania imekuwa ikiuza bidhaa nyingi zaidi Kenya kuliko inazoagiza
kutoka nchi hiyo,” alisena na kuongeza:
“Namsihi Waziri wa Biashara na Viwanda nchini
afuatilie suala hili na kuzungumza na mwenzake wa Kenya, ili waondoe vikwazo hivi
vya biashara ambavyo havina maana yoyote na vinazuia raia wa kenya kupata
bidhaa nafuu za Tanzania.”
Zitto alisema viwanda vingi vya Kenya
hutegemea malighafi ya Tanzania, hivyo kuzuia gesi hiyo na kuendelea kuagiza
malighafi za kuendesha viwanda vyao, ni sera ya Kenya kuifanya Tanzania chanzo
cha malighafi tu na si cha bidhaa zilizoongezwa thamani.
Alisihi Serikali kutokubaliana na hilo
na badala yake ifanye mazungumzo mara moja na ya Kenya ili Watanzania wanaouza
gesi hiyo Kenya waendelee kuiuza na kutumia bandari ya Dar es Salaam.
“Kama Serikali ya Kenya itaendelea na
msimamo wake, basi Tanzania ichukue msimamo kama huo kwa bidhaa za Kenya kama
maziwa, ambayo yamejaa kwenye soko letu,” alisisitiza Zitto.
0 comments:
Post a Comment