Celina Mathew
Dk Hellen Kijo-Bisimba |
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), kimeeleza kushitushwa na matukio yanayoendelea nchini, likiwamo la
waandishi wa habari kupigwa kwenye mkutano wa CUF na kumpa mapendekezo matatu
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini katika kuboresha demokrasia nchini.
LHRC imeeleza kwamba matukio hayo yanachochea
uvurugaji amani na kumomonyoa misingi ya demokrasia iliyojikita nchini.
Mapendekezo hayo ni pamoja na kumtaka Msajili
wa Vyama vya Siasa kuhakikisha ustawi mzuri wa vyama kwa kutatua migogoro ndani
na baina ya vyama ili kuepusha matukio ya uvunjifu wa amani na kudumisha ustawi
wa demokrasia.
Mengine ni Serikali kuhakikisha usalama
kwa raia wanapokuwa kwenye shughuli zao, ili kuepusha hofu kwa wananchi na vyama
kutumia uhuru wao kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa bila kusababisha
uvunjifu wa amani.
Akizungumza Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kwa kiasi kikubwa
mlolongo huo wa matukio ukiendelea unaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
“Tukio la uvamizi kwenye mkutano wa
ndani wa CUF uliosababisha kupigwa na kujeruhiwa kwa wanachama na waandishi wa
habari Mabibo, Kinondoni, limezidi kuzua mjadala katika jamii juu ya hatima ya
hali ya usalama kwa Taifa. Tunatoa pole kwa waandishi wa habari, viongozi na
wanachama wa CUF,” alisema.
Alisema wao LHRC wanaona ni ukiukwaji
mkubwa wa misingi ya demokrasia kwa kuzingatia aina ya shughuli iliyokuwa
ikiendelea na kwamba tukio hilo limezua hofu juu ya usalama wa wanahabari
wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao jambo ambalo linazorotesha haki
ya kupata taarifa.
“Tunaitaka Serikali kutofumbia macho
matukio haya yanayoota mizizi kwani kwa kufanya hivyo ni kuhalalisha vitendo
vya kihuni na kuruhusu uvunjwaji wa sheria kiholela na tunatamani jamii yenye
kuheshimu na kulinda haki za binadamu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment