Leonce Zimbandu
Abdul Kambaya |
WAKATI Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba akilaani waandishi wa habari kuvamiwa na kushambuliwa, Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, imemkamata Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na
Mawasiliano kwa Umma wa Chama hicho, Abdul Kambaya.
Kambaya alikamatwa jana kwa tuhuma za
kuhusika na vurugu hizo zilizotokea kwenye mkutano wa waandishi wa habari na
viongozi wa chama hicho wilaya ya Kinondoni hivi karibuni.
Alikamatwa wakati pia Profesa Lipumba akiwasilisha
barua yake kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil
Makunga, ikilaani kuvamiwa kwa waandishi wa habari katika tukio hilo.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda
hiyo, Simon Sirro alisema Kambaya ni miongoni mwa watu saba waliokamatwa kutokana
na vurugu kwenye mkutano huo.
Wengine kwa mujibu wa Kamanda Sirro ni
Hamisi Abdallah na Mtawa Rashidi, aliyetajwa kuwa mlinzi wa Profesa Lipumba na kwamba
upelelezi umekamilika na jalada la uchunguzi limewasilishwa kwa Wakili wa Serikali
tayari kufungua kesi mahakamani.
Kamanda Sirro alisema kesi zitakazofunguliwa
dhidi yao ni mbili; ya kuvamia na ya kushambulia na kwamba majalada ya kesi
zote yamewasilishwa kwa wakili huyo ili kufungua kesi baada ya kujiridhisha na
upelelezi uliofanywa na Polisi.
“Tunaomba aliyemkata panga mwenzake aliyefahamika
kwa jina la Mohamed kujisalimisha Polisi, kwani hawezi
kukimbia mkono wa Serikali, atapatikana tu,” alisema.
Aprili 22, watu watano wakiwa kwenye
gari lenye nembo na bendera za CUF, walivamia mkutano huo kwenye hoteli ya
Vinna wilayani Kinondoni na kufanya vurugu.
Miongoni mwa watu hao, mmoja aliyekuwa
amejifunika uso na kofia, alichomoa bastola na kutishia huku mwingine
akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na wenzake na kusababisha wananchi wamzingire
na kumshambulia.
Awali katika ufafanuzi wake, Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema tukio hilo ni la 13 dhidi
ya upande unaomwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad,
lakini vyombo vya Dola viko kimya.
“Baada ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa
kimya ili kuona kama polisi watasema chochote ila imekuwa tofauti, wako kimya
tu,” alidai.
Kuhusu barua ya Profesa Lipumba kwa
uongozi wa TEF, Mwenyekiti huyo wa CUF alisema yeye binafsi na kwa nafasi yake
katika chama hicho, analaani kitendo cha waandishi wa habari kupigwa wakiwa
kazini.
Alisema yeye na viongozi wenzake,
wanaamini katika siasa za demokrasia za ujenzi wa hoja na anatambua na
kuthamini umuhimu wa vyombo vya habari katika kukuza demokrasia na uwajibikaji
wa vyama vya siasa na vyombo vya Dola.
0 comments:
Post a Comment