Hussein Ndubikile
Mussa Shabani |
SHEKHE wa Mkoa wa Dodoma, Mussa Shabani,
ameiomba Serikali kuendeleza vita dhidi ya dawa za kulevya ili kudhibiti
mmomonyoko wa maadili katika jamii na upotevu wa nguvukazi ya Taifa.
Alitoa mwito huo akiwa Dar es Salaam
baada ya kumalizika kwa kongamano la mmomonyoko wa maadili na athari za dawa za
kulevya lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya.
Alisema vita hivyo havipaswi kukoma na
badala yake Serikali iwachukulie hatua za kisheria watakaoibainika kujihusisha
na matumizi na biashara hiyo, huku akisisitiza viongozi wa dini kutoa
mafundisho kwa waamini wao dhidi ya athari ya dawa hizo.
"Tuhakikishe kila mtu anakuwa
mlinzi ndani ya familia na jirani zake tusiachie Serikali pekee, kwani vita hivyo
ni jukumu la kila mmoja wetu," alisema Shekhe Shabani.
Alisisitiza kuwa endapo jamii
itashuhudia watu wanaotumia na kuendesha biashara ya dawa za kulevya wanachukuliwa
hatua kwa mujibu wa sheria za nchi kasi ya vitendo hivyo viovu itapungua.
Aliongeza kuwa asilimia kubwa ya vijana
ndio walioathiriwa na dawa hizo hali inayochangia mmonyoko wa maadili na kutaka
wazazi kuwaangalia kwa umakini ili kuwaepusha wasijiingize kwenye utumiaji na uuzaji
dawa hizo.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata
Taifa, Shekhe Hamis Mataka alisema Baraza litaendelea na programu ya umuhimu wa
kupambana na dawa hizo itakayoanzia ngazi ya Msikiti katani, wilayani hadi mkoani.
Shekhe Mataka alisema Bakwata itazindua
kitabu kitakachoitwa Kiongozi kikiwa na mafundisho ya kujenga jamii kimaadili
na kupambana na dawa za kulevya.
0 comments:
Post a Comment