Ahmed Makongo, Simiyu
TAKWIMU zinaonesha kuwa takribani wanafunzi 15 hadi 18 wa
kike kati ya 40 wanaojiunga na kidato cha kwanza wilayani Busega mkoani Simiyu
kila mwaka hukatisha masomo kwa sababu ya ujauzito.
Mbunge wa Busega Dk. Raphael Chegeni (CCM), alibainisha
hayo katika mahojiano na mwandishi wa
habari hii yaliyohusu masuala mbalimbali ya kimaendeleo jimboni humo, ikiwa ni
pamoja na kutaka kujua hali ya elimu.
Dk. Chegeni alisema kuwa kati ya wanafunzi wa kike 40
wanaoandikishwa kuanza kidato cha kwanza kila mwaka, takribani wanafunzi 15
hadi 18, wamekuwa wakikatisha masomo yao kwa sababu za ujauzito.
“Jambo hilo ndilo linalofanywa mtoto wa kike ashindwe
kufikia malengo aliyojiwekea maishani mwake,” alisema
Katika kukabiliana na suala hilo, mbunge huyo alisema
ameamua kuanzisha mkakati kabambe wa utekelezaji wa ujenzi wa hosteli za
wasichana katika shule zilizoko pembezoni mwa jimbo hilo, ili kuwanusuru watoto
hao wa kike.
“Ni hali ya kutisha sana maana kati ya watoto 40
wanaoandiskishwa kuanza kidato cha kwanza kati yao 15 hadi 18 ukatisha masomo
yao. Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo, nimeamua kuanzisha mkakati kabambe wa
kujenga hosteli kwenye shule zilizoko pembezoni mwa jimbo letu hili
tuweze kuwanusuru hawa watoto wetu wa kike,” alisema.
Alisema kuwa watoto wa kike wamekuwa wakienda ama kutoka
shuleni kwa kutembea kwa miguu, umbali mrefu, ambapo wakiwa njiani wamekuwa
wakikumbana na vishawishi vingi kutoka kwa wanaume.
Alisema kwa sababu hiyo, ameamua kusimamia ujenzi wa
mabweni ya wasichana ili watoto hao walale shuleni badalaya kutembea umbali huo
na kuendelea kupata vishawishi.
Dk. Chegeni alitaja shule ambazo tayari zimeshaanza
utekelezaji wa mradi huo wa hosteli za wasichana kuwa ni Sekondari ya Ngasamo.
Alisema kuwa shule hiyo imekuwa ikipokea wanafunzi wa
kata mbili za Imalamate na Ngasamo yenyewe.
Alisema kuwa mradi huo wa hosteli pia utatekelezwa katika
kata nyinginezo jimboni humo na kuongeza kuwa pia shule ya sekonmdari Mkula
itakuwa imeingia katika mkakati huo hivi karibuni.
“Shule nyingine ambazo ziko kwenye mkakati huu wa
kujengewa hosteli za wasichana ni Mkula, Malili, Kabita na Sogesca,” alisema.
Alisema kuwa wapo wadau mbalimbali wa maendeleo
ambao wamekuwa akiwatafuta kwa ajili ya kuchangia katika miradi ya maendeleo
ukiwemo ujenzi wa mabweni hayo.
Aliwataja baadhi ya wadau hao kuwa ni Shirika la Hifadhi
za Taifa (Tanapa), Ubalozi wa Ireland, Canada na serikali kwa ujumla.
Dk. Chegeni pia alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya
wanaume wakiwemo walimu wanaowarubuni watoto wa kike na kufanya nao mapenzi,
ambapo alisema kuwa katika jimbo hilo hawataki kuona mchezo huo unaendelea
kuwepo.
Alisema kuwa wanaume wa aina hiyo wasithubutu kufanya
mchezo huo, ikiwa ni pamoja na kuwataka walimu kutekeleza wajibu wao wa
kufundisha watoto na kufuata maadili ya kazi yao ipasavyo na siyo vinginevyo.
Aidha, aliwaomba wazazi na walezi kutoa ushirikiano wa
kutosha kwa vyombo vya dola kuhakiskisha wanaume wanaokatisha masomo ya watoto
wao kwa kuwapatia ujauzito wanachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwa ni
pamoja na kutoa ushahidi mahakamani pindi wanapohitajika na chombo hicho cha
kisheria.
Alisema kuwa wakati wote anakuwa mstari wa mbele
kuhamasisha jamii kuwekeza kwenye elimu, ambapo yeye binafsi amekuwa akitoa
misaada mbalimbali kwenye sekta ya elimu,ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa
vitabu kwenye shule ili kuhakikisha kila mwanafunzi anajitosheleza kwa kuwa na
kitabu chake cha kujifunzia.
Kuhusu suala la madawati alisema kuwa wananchi
walihamasika sana na kuhakikisha changamoto hiyo inamalizika na kila mwanafunzi
anasoma akiwa amekaa kwenye dawati.
Alisema suala la maendeleo jimboni humo linagusa sekta
mbalimbali ikiwemo ya elimu, maji, afya, miundombinu pamoja na miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Dk Chegeni, miradi ya maji imetekelezwa na
inaendelea kutekelezwa jimboni humo, ikiwa ni pamoja mradi wa maji
uliotekelezwa katika kijiji cha Lukungu na kwamba pia miradi mingine ya maji
ikiwemo ya visima virefu nay a bomba kutoka katika ziwa Victoria inaendelea
kutekelezwa katika maeneo mbalimbali jimboni humo.
Alisema kuwa mkakati wake mwingine ni kuhakikisha
wananchi wote hususan akinamama wanajiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali, ili
waweze kujiinua kiuchumi, sanajali mkakati wa kuwepo na chuo cha ufundi jimboni
humo, ili wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari na kushindwa
kuendelea waweze kujiunga kwenye chuo hicho na kujipatia ujuzi wa fani
mbalimbali na hatimaye kujiajiri wao wenyewe ama kuajiriwa.
Mbunge huyo alisema kuwa katika suala la maendeleo ndani
ya jimbo hilo hakuna cha itikadi za vyama vya siasa na aliwaomba wananchi wote
jimboni humo, kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha wanajiletea maendeleo,
kwa kushirikiana na serikali hii ya awamu ya tano chini ya rais wetu Dk. John
Magufuli.
0 comments:
Post a Comment