Sharifa Marira, Dodoma
Dk Jakaya Kikwete |
KIKAO cha kwanza cha Bunge la 11 jana
kilisimama kwa dakika 10 baada ya wabunge bila kujali itikadi zao za kisiasa kusimama
huku wakipiga meza zao kumshangilia Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye
alikwenda bungeni kushuhudia mkewe, Mama Salma akila kiapo cha ubunge.
“Tumekukumbuka, ingia ndani utusalimie,
njoo huku ndani utusalimie.” Ni baadhi ya kauli zilizotolewa na wabunge hao
baada ya Spika Job Ndugai kumtambulisha Rais mstaafu aliyekuwa ameketi kwenye
ukumbi wa wageni wa Spika, muda mfupi baada ya Salma Kikwete kula kiapo.
Wakati wabunge hao wakimshangilia, Rais
Kikwete aliyeambatana na mmoja wa watoto wake, Ally, alikuwa akitabasamu na
kuwapungia mkono wawakilishi hao wa wananchi, ambao baadhi yao waliwasha vipaza
sauti na kutoa hisia zao kwa Rais huyo wa Awamu ya Nne aliyemaliza muhula wa
pili wa utawala wake Novemba 2015.
Wabunge
Wabunge waliozungumza na gazeti hili
baada ya kikao hicho kuahirishwa, walitaja sababu za kumshangilia Kikwete ikiwamo
wakati wa utawala wake uchumi kuwa mzuri, kutokuwepo kwa demokrasia katika
utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano na kuminywa kwa uhuru katika masuala
mbalimbali.
“Haijawahi kutokea tangu niwe Mbunge.
Hiki ni kipindi changu cha nne kwa mgeni kushangiliwa namna hii,” alisema
Ndugai wakati shangwe za wabunge hao zikiendelea.
Wakati shangwe hizo zikiendelea, Ndugai
aliwataka wabunge kusimama na kumshangilia Rais huyo mstaafu kwa maelezo kuwa
kufanya hivyo ni kumpa heshima kubwa, ombi ambalo lilitekelezwa bila vikwazo na
wabunge hao, hata mawaziri.
‘’Kwa makofi hayo sasa naomba mumpe
heshima mpigieni makofi mkiwa mmesimama,’’ alisema Ndugai ambaye alichombeza: “Inawezekana waliommiss
(waliomkumbuka) nao wapo,” kuonekana kurejea tungo za wimbo uliozua utata
unaoitwa ‘Wapo’ ulioimbwa na msanii Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’.
Wimbo wa msanii huyo unaokosoa mambo
mbalimbali ulipigwa marufuku na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), kabla ya
Rais John Magufuli kutoa kauli ya kutaka uendelee kupigwa sambamba na msanii
huyo kuachwa huru, ikiwa ni saa 24 tangu akamatwe na polisi kutokana na
mashairi ya wimbo huo.
Kauli ya JK
Wakati hayo yakiendelea, Kikwete
alizungumzia ujio wake bungeni na kubainisha kuwa sasa ni zamu yake kumuunga
mkono mkewe kwa sababu wakati akiwa Rais, Mama Salma alimuunga mkono.
“Leo asubuhi nimeshuhudia kiapo cha mke
wangu, Mheshimiwa Salma Kikwete kuwa mbunge wa kuteuliwa bungeni mjini Dodoma.
Ni zamu yangu kumuunga mkono,” alinukuliwa Kikwete katika akaunti yake ya Twitter.
Mama Salma ambaye ni Mwenyekiti wa WAMA,
alipotakiwa kueleza sababu za Rais Kikwete kushangiliwa, alisema: “Inaashiria
kuwa Tanzania ni moja.
“Nashukuru wabunge kwa kunipokea vizuri,
naamini tutafanya kazi nzuri kwa kushirikiana, shangwe na vigelegele vya leo
(jana) vinaonesha Tanzania ni moja kwa kuwa zimetoka pande zote.”
Kauli za wabunge
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa (Chadema) alisema shangwe hizo zinaashiria kuwa wabunge wamewakilisha wananchi
wao kutoa hisia zao kwa Serikali ya Awamu ya Tano, ijue kwamba watu wanakumbuka
walikotoka.
‘’Ile ilikuwa salamu kwa Magufuli, tunamkumbuka
Kikwete, ambaye aliacha uchumi mzuri, mishahara ilikuwa inalipwa kwa
wakati, watumishi walikuwa wanapanda vyeo, lakini sasa mambo yamekuwa ya hovyo
kiwango chake aliyemwachia amekishusha,” alisema Msigwa.
Alisema Magufuli amedidimiza demokrasia,
hafuati taratibu za bajeti ananunua ndege bila Bunge kuidhinisha, amehamia Dodoma
bila Bunge kuidhinisha, hivyo ni lazima Bunge linalobanwa lioneshe hisia.
“Tumemkumbuka sana pamoja na kwamba
hakuwa mzuri kihivyo, lakini ukimlinganisha na Magufuli anamwacha mbali mno,
tulikuwa tunamtumia salamu kwamba Magufuli Watanzania waliingia ‘choo cha kike’,
mambo ya hovyo sasa,” alisema Msigwa.
Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya
(Chadema) alisema Kikwete alishangiliwa kutokana na namna ya uongozi wake,
hivyo Watanzania wengi wamemkumbuka, kwani alikuwa Rais mchangamfu kwa watu
wake, alipenda kupokea ushauri hata kama anatukanwa.
“Tuna kila sababu ya kumkumbuka Kikwete
na kumshangilia, ndiyo maana mliona pande zote zilishangilia, hivi ndivyo
wananchi walivyo, kwani sisi tunawakilisha wananchi na tulichoonesha ndizo
hisia za Watanzania wengi,” alisema Bulaya.
Alieleza kipindi cha Kikwete vyama vya
siasa vilikuwa na uhuru wa kufanya kazi zao kwa mujibu wa sharia, alikuwa
anapambana na ufisadi kwa kuruhusu watu kuainisha maeneo yenye ubadhirifu,
lakini sasa kila kitu kimeminywa
Alisema: “Kikwete tunamkumbuka kwa kweli,
japokuwa hakuwa mkamilifu kwa asilimia 100 lakini ukimlinganisha na Magufuli
hata ukiwaweka hapo Watanzania wengi watamchangua yeye, tunakumbuka uhuru wa
kujieleza, uhuru wa Bunge na vyombo vya habari, uchumi unayumba yaani hakuna
kuzuri.
“Napata shida mno mtu akisema Serikali
inapambana na ufisadi wakati haitaki wananchi waeleze maeneo yenye ubadhirifu,
akitokea mtu kueleza anaonekana adui wa Serikali, Kikwete alijitahidi kuacha
watu wamwoneshe mafisadi na aliwawajibisha kupitia Bunge.”
Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza
(Chadema) alisema kitendo cha kumshangilia Kikwete kina tafsiri
nyingi, lakini Serikali inataka kuendesha nchi kibabe, japokuwa wananchi
wanapinga.
Kikwete hakuingilia Bunge, aliliacha
lifanye kazi yake, hakuwa anasimama kutetea viongozi wanapotakiwa kuwajibishwa
kama inavyotokea sasa katika Serikali.
“Viongozi awamu hii wakitaka
kuwajibishwa Rais anasimama anatetea, Rais amekuwa akidhalilisha Bunge, Kikwete
hakuyafanya hayo, aliruhusu demokrasia na uhuru utawale, sasa tunarudishwa
nyuma miaka 50, hivyo wabunge walimshangilia kuonesha hisia zao kwake, japo
hakuwa mkamilifu lakini alifanya mengi mazuri,” alisema Peneza.
Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta (CCM)
alisema wabunge wamemkumbuka Kikwete kwa kazi nzuri aliyofanya wakati akiwa
Rais lakini pia walishangilia kwa kuwa wengi hawajamwona siku nyingi.
“Nimemkumbuka kwa kutujengea barabara
inayounganisha Tabora na mikoa mingine hali inayotusaidia
kusafiri kirahisi lakini pia
wabunge wengine huenda hawajamwona kiongozi wao
aliyeongoza kwa miaka 10 hivi karibuni, ndiyo maana walimshangilia,” alisema
Sitta
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara
(Chadema), alisema Kikwete anakumbukwa kwa mambo mengi mazuri, ukiwamo uhuru
kwa vyama vya siasa kufanya kazi zao na kukaa kuzungumza nao.
Bunge lilikuwa huru kufanya kazi zake
tofauti na sasa, ambapo linaminywa kufanya kazi zake, kwani kamati nyingi
zinapangiwa kazi za kufanya haziko huru ndiyo maana baadhi ya wenyeviti
wamejiuzulu.
“Kikwete alishangiliwa kwa mapenzi ya
dhati na watu wamekumbuka uhuru ambao alikuwa anautoa na sasa umeminywa, biashara
haziendi, uchumi unadidimia, wabunge hawafanyi kazi zao kama inavyotakiwa vitu
vingi havieleweki,” alisema Waitara na kuongeza:
“Serikali ya Kikwete ilikuwa haina
ubaguzi, mtu yeyote hata kama ni rafiki yake akiharibu anatolewa, lakini Serikali
hii kuna mtu ameghushi vyeti anatumia jina la mtu mwingine, lakini Magufuli
anaambiwa na anasimama kumtetea hadharani, ni lazima watu tumkumbuke Kikwete.”
0 comments:
Post a Comment