Suleiman Msuya
Maalim Seif Sharif Hamad |
VIONGOZI na wanachama wa CUF wakiongozwa
na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho (JUKECUF), Fatma Fereji wamesema
wapo tayari kukabiliana na njama ovu dhidi ya chama hicho na kwamba watakilinda
kwa gharama zozote zile.
Wanachama hao waliyasema hayo wakati wa
ziara ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alikuwa katika ziara ya
siku 10 katika kisiwa cha Unguja.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi
Habari Uenezi na Mahusiano, Mbarala Maharagande ilibainisha kuwa uamuzi huo
umetolewa na wana CUF ikiwa ni kutambua mchango wa katibu mkuu wao katika
kujenga chama.
Alisema katibu mkuu huyo amekuwa
akifanya ziara katika Kisiwa cha Unguja kuanzia Aprili mosi mwaka huu ziara ambayo
imekuwa na mafanikio makubwa.
Maharagande alisema wazo hilo la
kujitolea kulinda chama lilitolewa na wanachama wakati Maalim Seif akifanya
kikao cha majumuisho na tathmini katika ofisi ya CUF iliyoko Kilimahewa Wilaya
ya Mjini-Unguja.
“Ziara hiyo imepata mafanikio makubwa na
kufikia malengo yaliyowekwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF. Miongoni mwa
kazi alizofanya katika ziara hiyo ni pamoja na kukabidhi majukumu kwa waratibu
wa chama, ambapo jumla ya waratibu 4,727 walipatikana na ndipo uamuzi wa kukitolea
ulitokea,” alisema.
Aidha, alisema katika ziara hiyo Maalim
Seif aliweka mawe ya msingi katika maeneo sita, Baraza 14, majengo sita, na
kukabidhiwa viwanja viwili kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Chama.
Naibu mkurugenzi huyo alisema ziara hiyo
ilifanikisha kupatikana wanachama wapya 591 kati yao wanachama 124 walitoka
CCM.
Alisema katika kuhitimisha ziara hiyo,
chama kiliwapatia nishani maalum wanawake saba walio mstari wa mbele katika kutumia
rasilimali zao kwa ajili ya chama.
Katika hatua nyingine, Mahagande alisema
wabunge wa CUF wameendelea na ziara za kuimarisha chama katika wilaya
mbalimbali ikiwa ni sehemu ya utaratibu waliojiwekea kila wiki wakiwa bungeni
Dodoma.
Aliwataja baadhi ya wabunge ambao
walifanya ziara katika Wilaya ya Kondoa kuwa ni Masoud Abdallah Salim
(Mtambile), Saumu Sakala (Viti Maalum), Twahir Awezu Mohamed (Mkoani), Juma
Kombo Hamad (Wingwi), Mbarouk Salim Ali (Wete) na Mussa Mbarouk (Tanga).
Alisema wabunge hao wakiwa Kondoa walikutana
na kufanya vikao na viongozi wa kata, wajumbe wa kamati ya utendaji wilaya
pamoja na madiwani wa CUF na kuweka ratiba ya kuwafikia wanachama wengi zaidi.
Alisema wilaya na mikoani itakayofikiwa
hivi karibuni ni pamoja na Morogoro Mjini, Tanga, Pangani, Shinyanga,
Nyamagana, Ilemela-Mwanza, Lindi na Tabora.
Halikadhalika Mahagande alisema shauri
la msingi namba 23/2016 lililopo kwa Jaji Kihiyo dhidi ya Msajili Jaji Francis
Mutungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake
limepangwa kutajwa tena Aprili 24 mwaka huu.
Aidha, alisema shauri la wizi wa fedha
za ruzuku limepangwa kusikilizwa Aprili 20 mwaka huu kuhusu zuio la Lipumba na
wenzake kupewa fedha za ruzuku na Aprili 24 mwaka huu shauri la msingi mbele ya
Jaji Dyansobera.
0 comments:
Post a Comment