Asema
uvumilivu sasa basi
Fidelis Butahe
Maalim Seif Sharif Hamad |
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),
Maalim Seif Shariff Hamad ametaja hujuma tano zinazofanywa na dola kwa
kushirikiana na Profesa Ibrahim Lipumba kukisambaratisha chama hicho na Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akasema uvumilivu sasa umefikia mwisho.
Maalim Seif aliyetumia dakika 80
kuzungumza na wanahabari amesema wana ushahidi wa hujuma hizo za makusudi na
kwamba sasa litakalotokea anayestahili kulaumiwa ni watawala na vyombo vya
dola.
Kiongozi huyo ambaye amekatiza ziara
yake visiwani Zanzibar kwa kile alichokieleza kuja Dar es Salaam kuzungumza na
vyombo vya habari kueleza hujuma hizo, mbali na kuzitaja alisema hawezi kufanya
kazi na Profesa Lipumba kwa kuwa si mwanachama wa CUF.
“Nawaambia watawala walio nyuma ya
hujuma hizi chafu dhidi ya CUF, msitulazimishe kutusukuma kwenye ukuta. Tumevumilia
kiasi cha kutosha sasa basi, mlio nyuma ya hujuma hizi mtabeba dhamana ya
mnayoyaandaa,” alisema na kubainisha kuwa
atafanya ziara Dar es Salaam siku za hivi karibuni.
Katika hotuba yake ya dakika 80, Maalim
Seif akiwa sambamba na viongozi wakuu wa
CUF, alitoa wito kwa Watanzania wapenda demokrasia kusimama imara kulinda haki
huku akiania mkakati mpya wa sita unaofanywa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (Rita) kusajili bodi feki ya wadhamini ya chama hicho kufanikisha
njama ovu.
Alibainisha kuwa amepigania haki
Zanzibar kwa muda mrefu huku akilindwa na Mungu lakini siku zote waliompangia
njama wameondoka wao na kumuacha.
Alitaja Jeshi la Polisi, Hazina na Msajili
wa Vyama vya Siasa kuwa vinara wa hujuma hizo kutokana na kuendeleza mikakati
yao kwa kumtumia Profesa Lipumba, mwenyekiti wa CUF anayetambulika Ofisi ya
Msajili wa vyama vya Siasa.
Alisema zama za watawala kuwanyamazisha
Watanzania na kutaka matakwa ya mtu mmoja tu ndio yasimame, zimeshapita na
hazirudi tena.
“Huu ni wakati wa wapenda demokrasia na
amani nchini kusimama pamoja kulinda demokrasia yetu na kuzilinda taasisi zetu
zinazosimamia demokrasia yetu,” alisema.
“Kinachotafutwa hapa sio CUF.
Kinachotafutwa hapa ni kuua taasisi zetu zinazosimamia demokrasia. Tukiruhusu
kufanikiwa katika hili, hatutaweza kuzuia mengine. Tusiposimama pamoja
tutamalizwa mmoja mmoja tusitoa mwanya huo.”
CUF kiliingia katika mgogoro baada ya
Profesa Lipumba ambaye alijiuzulu wadhifa wake kuandika barua ya kutaka kurejea
jambo ambalo lilizua mgogoro na kusababishwa kufukuzwa uanachama lakini Ofisi
ya Msajili iliibuka na kueleza kuwa inamtambua kama mwenyekiti.
Kufuatia hali hiyo, CUF kupitia kwa
Baraza lake la Wadhamini walifungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo, huku
Profesa Lipumba ofisini na kukifanya chama hicho kuwa na taswira mbili tofauti
za uongozi.
Hujuma
tano
Akizitaja hujuma hizo, Maalim Seif alisema ya kwanza ni kutumika kwa
vyombo vya dola kumzuia kufanya shughuli zake Tanzania Bara huku vyombo hivyo
hivyo vikimlinda kwa nguvu Profesa Lipumba.
“Pili, kwa kutumia dola Profesa Lipumba
ameteka na kuvamia kwa nguvu ofisi za chama za wilaya mbalimbali nchini chini ya ulinzi wa dola. Tatu, ni wizi wa
fedha za ruzuku Sh milioni 369 uliofanywa kwa ushirikiano kati ya Lipumba, msajili,
hazina na benki,” alisema.
Alidai hujuma aya nne ni njama za
kujaribu kumuengua katika nafasi yake ya ukatibu mkuu huku ya tano ikiwa ni
Bunge kuridhia kupokea wagombea feki wa Bunge la Afrika Mashariki ambao
walishafukuzwa uanachama wa CUF.
Rita
yatajwa kuhusika
Alisema tangu zilipoanza njama za
kukihujumu CUF, kikwazo kinachowakwamisha vyombo hivyo kufanikiwa ni Bodi ya
Wadhamini ya chama hicho ambayo imechukua hatua za kukilinda chama kupitia
mahakama.
“Tuna taarifa zisizo na shaka. Kuna
shinikizo la kumtaka Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita kusajili wajumbe feki wa bodi
ya wadhamini ya CUF kwa kutumia majina yaliyowasilishwa na Lipumba ili kutimiza
malengo yao matano,” alisema Maalim Seif.
Aliyataja malengo hayo kuwa ni kuitumia
bodi hiyo feki kufuta kesi zote zinazomkabili mwenyekiti huyo, Msajili wa Vyama
vya Siasa, kufungua akaunti mpya ya Benki ili kuwezesha kupatikana fedha za
ruzuku, kumuondoa katibu Mkuu kwenye wadhifa wake na bodi hiyo kudhibiti Ofisi
za Makao Makuu ya CUF zilizopo Mtendani, Zanzibar.
“Wanataka kuhujumu majina halali
yaliyowasilishwa na kikao halali cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama kilichofanyika
makao makuu visiwani Zanzibar Machi 19, mwaka huu,” alisema.
Alisema bodi ya Wadhamini cha chama
hicho ilishasajiliwa tangu mwaka 1993 kwa kuzingatia Sheria ya Wadhamini na
kwamba kinachofanyika kila baada ya kipindi fulani ni kuweka kumbukumbu za bodi
hiyo.
Alisema CUF kimefanya mabadiliko
machache ya baraza hilo na kuyawasilisha RITA lakini Profesa Lipumba ametakiwa
kuandaa majina yake na kuyafikisha katika ofisi za wakala huyo kwa malengo
matatu.
Alisema kwa kutumia njama hizo watawala
wanadhani watakuwa wamekidhibiti CUF na kwamba watakuwa wamezima hoja za chama
hicho kupokwa ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Tunajua Msajili wa Vyama anaishawishi
Rita kukubali uhuni huu. Anaonekana ana maslahi binafsi katika hili. tunasubiri
uamuzi wa Rita ili tuone kama nao wanatumika,” alisema.
Uvumilivu
basi
Kuhusu kuvumilia kwa muda mrefu hujuma
na njama hizo alisema, “kama Rita watamtambua Lipumba litakalotokea watawala
watabeba dhamana. Siwezi kusema zaidi ya hapo.”
“Tumekuwa wapole na waungwana maana hii
nchi ya amani. Tungetaka machafuko nchi hii yangeshatokea tangu zamani.
Wasijisifu, si vyombo vya dola vinavyotunza amani ni CUF…, watu wakidhamiria
kufikia malengo yao utaua watanzania wote, utaua wachache tu.”
Alisema hata akikamatwa sambamba na
viongozi wengine wa chama hicho, wapo wanachama wengine wataendeleza mapambano
ya kudai haki, demokrasia na utawala wa sheria.
“Wapo wanaosema kuwa nawachelewesha ila
siku zote nimekuwa nikizuia jambo hili nikitegemea upande wa pili utaliona
hili. Kama watatufikisha tukabanwa na ukuta litakalotokea watajibu wao,”
alisema.
Alisema ikiwa Lipumba atachukua ofisi za
CUF Zanzibar, hawezi kuwazuia vijana kupambana ili jambo hilo lisitokee.
Amjibu
Lipumba
Alisema licha ya kufukuzwa Profesa Lipumba
amendelea kujiita mwanachama wa CUF sambamba na kuchukua majukumu kadhaa
yasiyomhusu ikiwa ni pamoja na kufukuza wanachama, kuunda mabaraza ya maamuzi na
kutumia fedha za chama.
“Siwezi kukaa na Lipumba kwani sio
mwanachama na uamuzi wa kumfukuza ushafanywa na vikao siwezi kuingilia” alisema.
“Profesa Lipumba anasema eti nashindwa
kufanya kazi zangu ataniondoa ajabu hii! Lini nimeshindwa kufanya kazi. Lini
mwenyekiti akampangia kazi Katibu Mkuu?”
Alisema hata kama Profesa Lipumba
angekuwa mwenyekiti halali hampi madaraka na kuchukua uamuzi kama anaoufanya
sasa.
Njama
ovu 10
Katika mkutano huo na wanahabari, Maalim
Seif alitaja mbinu 10 ovu zinazofanyika tangu Serikali ya Awamu ta Tano kuingia
madarakani.
Alizitaja mbinu hizo kuwa ni kupiga
marufuku mikutano ya kisiasa, kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge,
kuminya bajeti ya Bunge, kuwakamata na kuwafungulia mashataka wabunge, kuzipa
mahakama maagizo.
Nyingine ni kuwakamata watumiaji wa
mitandao ya kijamii na kuwafungulia mashtaka, kuwatisha wanahabari, kuwatisha
na kuwakamata wasanii, kuzitisha jumuiya za kiraia na wakuu wa mikoa na wilaya
kujipa mamlaka kinyume na sheria.
0 comments:
Post a Comment