Grace Gurisha
RAIA wa Kenya, Mary Amukowa, anayekabiliwa na kesi ya
kusafirisha wasichana 10 kutoka Tanzania kwenda Kenya kuwafanyisha biashara ya
ngono, ameiomba Mahakama imwache huru kwa madai kuwa kesi hiyo ni ya
kutengenezwa.
Mary alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey
Mwambapa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakati akijitetea
dhidi ya kesi inayomkabili yeye, rafiki yake Jackline Milinga na Simon Mgawe.
Mkenya huyo alidai kuwa yeye ni mfanyakazi wa kampuni ya
simu ya Safaricom ya Nairobi, Kenya na aliajiriwa mwaka 2014 na alikuwa
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi.
Akiongozwa na Wakili Nehemia Nkoko, Mary alidai kuwa
Septemba 4 mwaka juzi akiwa na Jackline walisafiri kwa basi la Modern Coast
kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi, ambapo walikata tiketi wakakaguliwa mizigo
na hati zao za kusafiria bila matatizo.
Aliendelea kujitetea kuwa alikuja Dar es Salaam
kumtembelea Jackline na nchini hakuna mtu aliyekuwa anamfahamu zaidi ya huyo na
walifahamiana mwaka 2001 wakiwa Bujumbura, Burundi.
Mary alidai walipofika Namanga mpakani mwa Kenya na
Tanzania akiwa ameshagongewa muhuri wa
kutoka nchini akiwa kwenye foleni ya kusubiri kugongewa muhuri wa kuingia
Kenya, maofisa Uhamiaji wawili wa Tanzania walimkamata Jackline wakisema wana shaka
na hati yake ya kusafaria, kwa sababu ilikuwa ni ya kidiplomasia na baadaye
wakabaini kuwa halali.
“Mimi niliomba tuachwe huru, walituchukua maelezo,
wakatupa na hao wasichana 10, tulikaa siku nne Uhamiaji Makao Makuu lakini tulipohamishiwa
Uhamiaji mkoa hawakuwa nao tena,” alidai Mary.
Pia alidai hajui wasichana anaotuhumiwa kuwasafirisha na
wala hakuwahi kuwaona hadi siku Zulfa, Lea, Angelina na Amina walipopelekwa
mahakamani kutoa ushahidi kwa upande wa mashitaka.
“Mashitaka haya ni ya uongo na kutengenezwa, sijawahi
kusafirisha binadamu yeyote, mimi ni mfanyakazi wa Safaricom naomba Mahakama
iniache kwa sababu tuhuma hizi ni za uongo,” alidai Mary.
Mgawe alidai tuhuma hizo si za kweli kwani hajawahi
kusafiri nje ya nchi wala kukusanya binadamu kwa lengo la kuwasafirisha, hivyo
aliomba Mahakama naye imwache huru.
Baada ya washitakiwa hao kutoa utetezi wao, pande zote
zilitakiwa kuwasilisha hoja za majumuisho za kuishawishi Mahakama iwaone wana hatia
au la kabla ya Mei 11 ambapo kesi hiyo itatajwa.
Jackline, Mary na Simon wanadaiwa kuwa Septemba 4 mwaka juzi,
Magomeni na Makumbusho waliajiri
wasichana 10 na kuwasafirisha.
Inadaiwa kuwa waliwaajiri Najma Suleiman, Leah Mussa,
Zulfa Ally, Rahma Mohammed, Salima Komba, Angelina Banzi, Leila Chorobi,
Elizabeth Nalimu, Amina Abdi na Sada Hussein na kuwasafirisha kutoka Tanzania kwenda Kenya kwa shughuli za
ngono, huku wakijidai kuwa waliwapeleka kufanya kazi.
Inadaiwa wasichana hao wana umri wa kati ya miaka 18 na
22.
0 comments:
Post a Comment