Suleiman Msuya
Kituo cha mabasi Ubungo |
HALI si shwari. Ndivyo unavyoweza kusema
baada ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kusisitiza kuanza mgomo
kesho iwapo hoja zao zitaendelea kupingwa na Serikali katika kikao kinachotarajiwa
kufanyika leo.
Katika hali isiyo ya kawaida chama hicho
kimetangaza rasmi kutokuwa na imani na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kwa madai ya kugoma kusikiliza hoja zao,
jukumu ambalo sasa amelivaa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mhandisi Edwin
Ngonyani aliyeahidi kuwa waziri atakutana na chama hicho leo.
Wamiliki hao wa mabasi pamoja na
wamiliki wa daladala mkoa wa Dar es Salaam (Uwadar) walikutana juzi kupinga Muswada
wa Sheria unaotarajiwa kuwasilishwa katika Bunge la Bajeti linaloanza kesho
mjini Dodoma.
Mgomo huo utahusisha mabasi yote ya
abiria yaendayo mikoani na nchi za jirani na yale yanayosafirisha abiria jijini
Dar es Salaam, maarufu kama daladala, kupinga mabadiliko ya sheria ambayo
Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imeyafanya.
Sumatra ilitunga muswada ambao
unatarajiwa kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kusomwa na kupitishwa kama
sheria, ambapo wamiliki hao wanasema hawakushirikishwa na ukipitishwa utakuwa
mwiba kwao.
Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu jana
alilieleza gazeti hili kuwa hawatambui ni kwanini mchakato wa sheria hiyo
haujawashirikisha ila wakati wa kanuni ndio wanaonekana kuwa wa muhimu.
Mrutu alisema taarifa za sheria hiyo
walizipata kupitia Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba ambapo waliwaita Dodoma
bungeni na Serikali ilivyohojiwa ni kwanini haijawashirikisha ilikaa kimya.
Alisema hawapo tayari kuona sheria hiyo
ikifanya kazi kwani imeonekana kukandamiza wasafirishaji huku wakiwa hawahusiki
kwa asilimia yoyote katika makosa mengine ya barabarani.
“Kesho sisi tunagoma kama hakutakuwa na
mazungumzo ya maana, kwani sheria ambayo tunailalamikia hatukushirikishwa
tuliitwa kwenye kanuni jambo ambalo si sawa,” alisema.
Kuhusu kupata wito wa waziri alisema
hadi anazungumza na JAMBOLEO hakuna taarifa yoyote ambayo walipata hivyo wao
wanaendelea na mchakato wa mgomo ili kupata ufumbuzi.
Msemaji wa Taboa, Mustapha Mwalongo
alisema wanachama wamechoka kunyanyaswa na kutosikilizwa hivyo kinachosubiriwa
kwa sasa ni mgomo.
Alisema juzi katika kikao cha dharura
wanachama walimjia juu mwenyekiti ambaye alionekana kukosa msimamo, hivyo
wameweka bayana iwapo kamati ya utendaji itawasaliti watachukua hatua ya
kuwaondoa.
Mwalongo alisema wamefanya jitihada
mbalimbali za kumwona waziri, lakini hakutaka kuwasikiliza hivyo wakati huu ni
wao kuonesha vitendo kutokana na makosa ambayo yamefanyika.
“Haiwezekani unatengeneza sheria ambayo
inasema dereva anatenda kosa mmiliki alipe au afungwe miaka minne wapi umeona
sheria ya hovyio kama hiyo hapa duniani,” alisema.
Alisema yapo makosa ambayo mmiliki
anaweza kuwajibika lakini si hili la makosa ya barabarani kama Serikali kupitia
Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumtra).
Msemaji huyo alisema sekta ya usafiri
inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya mabasi kulipa sh. 2,000 kila kituo
cha basi kilichopo kwenye halmashauri hata kama gari haishushi au kupakia.
Alisema kodi hizo wamekuwa wakivumilia
kwa muda mrefu ila kwa sasa maji yamefika shingoni na uamuzi ambao utachukuliwa
ni kusimamisha huduma hiyo.
“Kodi ni nyingi sana gari moja inalipa
hadi Sh. 28,000 kutoka Dar es Salaam hadi Arusha ndugu yangu mnyonge mnyongeni,
lakini haki yake mpeni tumenyongwa sana sijui tunafanya makosa kununua mabasi,”
alisema.
Akizungumzia kizungumkuti hicho Naibu
Waziri Ngonyani alikiri kusikia taarifa hizo kupitia vyombo vya habari na
kwamba amewasiliana na waziri wake na kukubaliana kukutana na wasafirishaji leo
jijini Dar es Salaam.
Alisema kinachoonekana ni kukosekana kwa
mawasiliano mazuri baina ya Serikali na wasafirishaji hivyo ni wakati muafaka
kuzungumza na kuachana na dhana ya kugoma kwani haina tija kwa nchi.
“Suala la mgomo halikubaliki popote
kabla ya mazungumzo, hivyo naamini watazungumza kesho na muafaka utakuwepo
tusubiri kesho,” alisema.
Ngonyani alisema amefanikiwa kuwasiliana
na Mwenyekiti wa Taboa, Mohamed Hood ambapo alimueleza kuwa wanachama
wamesisitiza kugoma.
Alisema mwenyekiti huyo alimueleza kuwa
alishindwa kudhibiti mkutano huo na kumuahidi kukutana na waziri ili kupata
muafaka.
Naibu waziri alisema wao katika serikali
wanazingatia ushirikishwaji katika kila jambo ambalo wanalifanya hivyo hayo
yanayosemwa kuwa hawajashirikishwa au hawatashirikishwa si kweli.
0 comments:
Post a Comment