*Imo pia Mahakama, Bunge, Wizara ya Maji
*Mabilioni yalipwa kwa marehemu, wasiokazi
Mwandishi
Wetu
IGP Mangu |
JESHI
la Polisi nchini limetajwa kuongoza kulipa mishahara watumishi wasiokuwa kwenye
utumishi wa umma kati ya taasisi za Serikali katika mwaka wa fedha 2015/16.
Ripoti
ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu matokeo muhimu kwenye
ukaguzi wa usimamizi wa rasilimaliwatu na mishahara kwa wizara, sekretarieti za
mikoa na balozi kwa mwaka wa fedha 2015/16 umelitaja Jeshi la Polisi kuongoza kati
ya taasisi 19 zilizobainika kuwa na tatizo hilo.
Taasisi
zinazokaribiana na Polisi zimetajwa na CAG kuwa ni Mahakama na Wizara ya Maji
na Umwagiliaji, huku Bunge likitajwa pia kuhusika.
Katika
ukaguzi wake, CAG alibaini kuwa taasisi 19 zililipa Sh bilioni 1.40 za
mishahara kwa watumishi 260 walioacha kazi, waliofariki dunia, wastaafu na
waliofukuzwa, fedha ambazo zilitakiwa kurejeshwa.
“Jeshi
la Polisi limelipa watumishi 139 wasiokuwa kwenye utumishi wa umma likitumia Sh
757,316, 000,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo ya CAG iliyotolewa wiki iliyopita
ikifafanua:
“Kati
ya fedha hizo, zilizorejeshwa ni Sh milioni 14. 03.”
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo, Idara ya Mahakama inafuatia kwa kulipa watumishi 27 ikitumia Sh 182,913,133 ya
tatu ikitajwa kuwa ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji iliyolipa Sh 63,324,829 kwa
watumishi 26 na kubainisha kuwa Mahakama tayari imerejesha Sh milioni 35.03 na
Wizara ya Maji Sh milioni 47.04.
Ilibainisha
kuwa malipo ya mishahara kwa wafanyakazi wasio kwenye utumishi wa umma yalifikia
Sh 1,400, 554,592.
CAG
alisema mishahara hiyo ililipwa kati ya mwezi mmoja hadi 72 huku taasisi hiyo
ya ukaguzi ikieleza malipo hayo kuwa kinyume na kanuni ya 113 ya kanuni za
Fedha za Umma za mwaka 2001 (zilizorekebishwa mwaka 2004) inayoagiza maofisa masuuli
watunze nyaraka za watumishi ili wanaolipwa wawe ni waliopo na wanafanya kazi.
“Taasisi
nyingine ni Bunge ambapo watumishi wawili walilipwa Sh milioni 2.5, Sekretarieti
ya Mkoa wa Kigoma watumishi 12, zaidi
ya Sh milioni 150.5, Zimamoto watumishi wanne Sh milioni 2.8 na Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia watumishi wanane, malipo zaidi ya Sh milioni 62.5.
Pia
alitaja Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto watumishi wanane malipo zaidi
ya Sh milioni 18.5 na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, watumishi
wanne Sh milioni 5.3.
Ripoti
hiyo ilibainisha taasisi zingine kuwa ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi mtumishi mmoja, Sh milioni 22.6 na zilirejeshwa Sh milioni 10,
Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera watumishi wanane Sh milioni 12.1 na marejesho ni
Sh. milioni 6.7.
Mikoa
mingine ni Shinyanga mtumishi mmoja Sh milioni 43, marejesho Sh milioni 22.25,
Geita wanne, malipo ni Sh milioni 26.6 na marejesho Sh milioni 17.3, Rukwa watumishi
sita, malipo zaidi ya Sh milioni 2.7, Ruvuma wanne Sh milioni 15.8 na Tanga
watumishi watatu Sh milioni 3 zilirejeshwa Sh. milioni 1.3.
Ripoti
ya CAG ilitaja pia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kulipa mtumishi
mmoja Sh milioni 22.4, mkoa wa Manyara malipo Sh. milioni 1.5 kwa mtumishi
mmoja huku Mtwara ikilipa mmoja Sh milioni 3.6.
Wabunge
Akitoa
maoni kuhusu ripoti ya CAG, Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), alisema pamoja
na makusanyo kuwa makubwa kumekuwa na nidhamu ndogo ya matumizi ya fedha.
Kwamba
ingawa CAG hajaeleza sababu, lakini hali hiyo inatokana na Serikali kukosa
nidhamu katika matumizi.
Alibainisha
kuwa kiasi cha fedha kinachotengwa kinakuwa kikubwa lakini matumizi yanapelekwa
kwingine akitolea mfano wa ununuzi wa ndege ambao fedha zake hazikuwa
zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2016/17.
Alitilia
shaka kuwa fedha ambazo zimeainishwa kutumika katika matumizi yanayotiliwa shaka
ya kuwepo kwa hali ya rushwa, inawezekana zikawa ndizo zinatumika kuendeshea
miradi mikubwa isiyo kwenye bajeti, kwani haijapitishwa kwa utaratibu wa Bunge.
Aidha,
alisema kuhusu suala la mashirika ya umma kuna hatari kubwa ya kufilisika
kutokana na Serikali kukopa fedha nyingi na kuzipeleka kwenye matumizi yake.
Mbunge
wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM)
alisema hajamaliza kuipitia ripoti hiyo, hivyo hawezi kuzungumza kwani
anahitaji muda wa kuisoma vizuri na kwa umakini akieleza kuwa anatarajia
mchango wake kusikika akichangia bungeni.
“Siwezi kuzungumza chochote, bado
naendelea kuisoma, mchango wangu nitautoa bungeni,” alisema Bashe.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT)
alisema ripoti hiyo ni kubwa na imegusa maeneo mengi, akiyataja mikataba ya
madini, Tanesco, misamaha ya kodi na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Aidha, alisema hawezi kuzungumza zaidi
sasa kwani ripoti ni kubwa na hajui ajikite eneo gani. Kutokana na hali hiyo,
Zitto alisema anahitaji muda kuisoma vizuri.
“Huwa napenda kutoa mchango wangu
mapema, lakini kwa sasa CAG amegusa maeneo mengi, hivyo nashindwa nijikite
wapi, nahitaji muda kwanza niisome vizuri,” alisema Zitto.
0 comments:
Post a Comment