PYONGYANG, Korea Kaskazini
Kikosi cha Jeshi cha Korea Kaskazini |
KIONGOZI wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un
ameanika kikosi chake maalumu cha kijeshi kwa mara ya kwanza mwishoni mwa wiki
hii, kama hatua ya makusudi ya kumwonesha Rais wa Marekani Donald Trump uwezo
wake kijeshi.
Kikosi hicho chenye askari waliofunzwa
barabara kilipita mitaani jijini hapa Jumamosi wakiimba nyimbo za kizalendo
huku wakiwa wamekumbatia bunduki zao zenye uwezo pia wa kurusha mabomu.
Askari hao wanaosemekana kuwa na vifaa
bora vya kivita ndani ya Jeshi la Watu wa Korea, walivalia pia miwani ya kuonea
usiku iliyofungwa kwenye kofia zao za chuma huku bunduki zao zikining’inia
vifuani.
“Mara tu Kamanda Mkuu Kim Jong Un
atakapotoa amri, watasonga mbele kwa lengo la ‘kuuchoma mkuki moyo wa adui kwa
kasi ya radi juu ya Mlima Paektu (kilele kirefu kuliko vyote nchini)’,”
mtangazaji wa televisheni ya Taifa alisikika akitangaza.
Kujitokeza kwa kikosi hicho kwenye
sherehe za Siku ya Jua mwishoni mwa wiki, kulikuja huku kukiwa na msuguano na
Marekani na Rais Trump ambaye amekataa kukanusha mpango wake wa kuishambulia
Korea Kaskazini kabla Rais Kim
hajabonyeza kiwambo cha kufyatulia makombora ya nyukilia.
Vikosi maalumu nchini viko tayari
kulinda nchi hii dhidi ya majeshi ya Marekani, ambayo yanafanya mazoezi ya
kumng’oa madarakani Kim mara mapigano yatakapoanza, mchambuzi wa shirika la
habari la Yonhap nchini anadai.
Taarifa ya makao makuu ya Jeshi la
Marekani – Pentagon, iliwaelezea wanajeshi hao wa Korea Kaskazini kama miongoni
mwa waliopewa mafunzo mazuri, wenye vifaa bora, wanaolishwa vizuri na wenye
motisha ya hali ya juu ndani ya Jeshi la nchi hii, CNN iliripoti.
Ilisema kikosi hicho kisiochoonekana
mara kwa mara, kinachosemekana kuendesha operesheni za siri nchini, kinaonekana
kuandaliwa kwa ajili ya operesheni nzitonzito na kujilinda dhidi ya
mashambuilizi kutoka nje.
Taarifa hiyo inaendelea kusema, kwamba vikosi
hivyo maalumu huendesha mambo yao katika vitengo maalumu, ikiwa ni pamoja na
utambuzi, mashambulizi ya angani na ya majini, makomando na utaalamu mwingine
wa kijeshi.
Ilibasihiri pia, kwamba Korea Kaskazini
imedhamiria kuendesha mapigano ya masafa marefu, ikitumia makombora ya nyukilia
yenye uwezo wa kuishambulia Marekani moja kwa moja.
0 comments:
Post a Comment