Leonce Zimbandu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka
mikakati mitano ya kuboresha ukusanyaji kodi ya majengo, ikiwamo kutathmini
majengo ili kupanga viwango rafiki vya kodi kwa walipakodi.
Mikakati mingine ni kuimarisha usimamizi
na ufuatiliaji wa ukusanyaji, kutoa elimu kwa jamii kuhusu ulipaji kodi, kushughulikia
pingamizi za kodi kwa wakati na kuboresha orodha ya uthamini ili kuwa na
takwimu sahihi.
Ofisa Msaidizi wa Huduma ya Mlipakodi ya
TRA, Maya Magimba alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana kuhusu umuhimu wa kodi.
Alisema kodi ni muhimu kwa Serikali kwa
vile inatumika kuendesha shughuli za kijamii, ukiwamo ujenzi wa miundombinu ya
barabara, zahanati na madarasa.
“Tutahakikisha nyaraka za usajili
zinatunzwa na mlipakodi kwa kufuata taratibu ili kuepuka usumbufu,”
alisema.
Alisema kodi ya majengo hulipwa kuanzia
Januari mosi hadi Machi 31 kila mwaka bila adhabu, na baada ya Aprili mosi
hulipwa na adhabu, kodi ya pango la ardhi hulipwa kuanzia Julai mosi hadi
Desemba 31 kila mwaka.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo na
Makazi, Mboza Maige alisema mwananchi au taasisi yenye nyaraka za umiliki
wa ardhi ya Serikali anapaswa kulipa kodi hiyo.
Alisema iwapo eneo litakuwa na
maendelezo ya jengo la kudumu na linatumika, mtu huyo atalazimika kulipa kodi
mbili.
0 comments:
Post a Comment