Celina Mathew
Rais Magufuli akizindua ujenzi wa reli |
RAIS John Magufuli ameweka jiwe la
msingi la ujenzi wa reli ya kisasa kwenye kituo cha reli cha Pugu, akisema yeye
ni dereva na hakuna wa kumyumbisha.
Magufuli jana alifanya uzinduzi huo utakaogharimu
Sh trilioni 2.7 hadi kukamilika kwake.
Ujenzi wa reli hiyo mpya ya kisasa awamu
ya kwanza ni wa kati ya Dar es Salaam na Morogoro itakuwa ya pili Afrika kwa mwendo kasi wa
kilometa 160 kwa saa, baada ya iliyoko Moroco.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais
Magufuli alijifananisha na dereva wa lori, akisema dereva mzuri siku zote
hapaswi kusikiliza muziki unaopigwa ndani ya gari, bali huangalia gari linakoelekea.
“Mimi ni dereva mzuri, nimepakia
waendaji wanaoimba, wanaotazama mbele, nyuma na ubavuni, kila mmoja anaimba
wimbo wake, lakini kazi yangu si kusikiliza nyimbo zao, bali kuhakikisha gari
linafika linakoenda. Nami nitaifikisha Tanzania inakostahili kufika kwa kuwa
wanaopiga kelele ni wapiga dili,” alisema Magufuli.
Alifafanua, kuwa alipoomba kura kwa
wananchi aliahidi kusaidia masikini kuondokana na hali hiyo na hakuna wa
kubadili ajenda.
“Wabunge waliahidi majimboni, hivyo
najua tunakokwenda, asitokee mtu akabadili ajenda tukaacha kujadili yaliyo
kwenye Ilani ya Uchaguzi, tukajadili mambo yasiyo na maendeleo,” alisema na
kuongeza:
“Mapambano ya kukuza uchumi na ufisadi
ni magumu yana milolongo, hasa unapobadili watu wachache waliozoea maisha ya
ufisadi kwa miaka 50 kwa kuwa Waswahili husema ‘samaki mkunje angali mbichi’,
mimi namkunja sasa kabla hajakomaa, bora walalamike wachache wengi wafurahi.”
Kauli ya Rais Magufuli imekuja huku
kukiwa na malalamiko kutoka kwa watu wa kada mbalimbali kuhusu utendaji wa
Serikali yake na hali ya maisha vikiwamo vitendo vya utekaji watu, vinavyoelezwa
kukithiri nchini.
Akizungumzia ujenzi wa reli hiyo, Rais
Magufuli alisema umepangwa kukamilika ndani ya miezi 30 ukihusu ujenzi wa
kilometa 300 ambazo kilometa 205 zitakuwa za njia kuu na 95 za reli ya
michepuko ya treni kupishana na kupanga mabehewa.
Rais Magufuli alisema mradi huo utakuza
biashara kati ya Tanzania na Burundi, Rwanda, Uganda na Sudan, na utarahisisha
kasi ya usafirishaji mizigo kutoka mikoa mbalimbali nchini, itakuza sekta
ya uchumi hususan za viwanda, mifugo,
madini na uvuvi.
Pia alisema utasaidia malighafi
kusafirishwa kutoka zinapozalishwa hadi viwandani, utakuza utalii kwa watu
wanaotoka Afrika Kusini na nchi zingine kwa kutumia treni, kutunza barabara na
kuongeza ajira.
Aidha, alisema walipotangaza zabuni, wakandarasi
40 walijitokeza, lakini kampuni ya Uturuki ilishinda hivyo mkandarasi ameshalipwa
Sh bilioni 300 kwa ajili ya kuanza kazi.
Aliwataka wakandarasi kuhakikisha
wanafanya kazi haraka kwa kuwa fedha zipo na ikiwezekana ukamilike kabla ya
miezi 30.
RAHCO
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni
Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Masanja Kadogosa alisema kutakuwa
na vituo sita vya abiria na vidogo sita vya kupishana treni.
Alisema treni zitaweza kusafiri kutoka
Dar es Salaam hadi Dodoma kwa saa mbili na baada ya kukamilika awamu zote tano
za ujenzi, zitaweza kufika Mwanza chini ya saa 10.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema kukamilika kwa mradi huo
kutaboresha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ya Tanzania (TPA) kutoa mizigo kwa
haraka na kufikia wateja, tofauti na ilivyokuwa awali, huku Watanzania 600,000 wakipata
ajira za moja kwa moja.
0 comments:
Post a Comment