Suleiman Msuya
MBIVU mbichi za wagombea wa Ubunge wa
Bunge la Afrika Mashariki zitajulikana leo wakati Bunge litakapotoa taarifa
rasmi.
Aidha, Bunge linatarajia kutangaza
ratiba ya Mkutano wa Saba wa Bunge la 11 ambao unatarajiwa kuanza kesho mjini
Dodoma.
Hayo yamesemwa na Ofisa Habari wa Bunge,
Owen Mwandumbya, wakati akizungumza na JAMBOLEO jana.
Mwandumbya alisema leo ndio watatoa
taarifa nzima kuhusu mchakato wa wabunge wa Bunge la EALA na taarifa kuwa kuna
wagombea wamekatwa yatajulikana.
“Kesho (leo) wagombea ubunge Bunge la
EALA watajulikana kwani mchakato mzima umefanyika naomba usubiri kesho hayo
ambayo yanasemwa yatajulikana,” alisema.
Aidha, Owen alisema leo wanatarajia
kutoa ratiba nzima ya Mkutano wa Saba wa Bunge la 11 ambao unatarajiwa kuanza
kesho na kubainisha kuwa moja ya kazi ambayo itafanyika ni kuchagua wabunge wa
EALA.
Mchakato wa kuwapata wagombea wa bunge
hilo umegubikwa na sintofahamu kulingana na utaratibu ambao umezoeleka wabunge
wa EALA wanatokana na chama chenye wabunge wengi, lakini katika kipindi hiki
hali imekuwa kinyume ambapo vyama vyote vyenye wabunge vimewasilisha wagombea.
Kuingia doa kwa sakata hilo kulianzishwa
na Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye aliandika
barua kwa Spika wa Bunge Job Ndugai kudai chama chake kina haki ya kuweka
mgombea.
Hali hiyo ilipelekea ACT-Wazalendo
kuwakilisha jina la Profesa Kitila Mkumbo, NCCR-Mageuzi Dk. Nderakindo Kessy
hali ambayo inazidi kuchanganya ni kipi kitafuata kwa maamuzi hayo.
Wagombea wengine wa vyama vya upinzani
ni Laurence Masha, Ezekia Wenje wa Chadema wakati Chama cha Wanachi (CUF)
kikiwasilisha majina ya Twaha Taslima, Thomas Malima, Habibu Mnyaa na Sonia
Magogo.
Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kwa wagombea ni Zainab Kawawa, Happiness Lugoko, Fancy Nkuhi, Happiness
Mgalula, Ngwaru Maghembe, Adam Kimbisa, Anamringi Macha na Makongoro Nyerere.
Aidha, chama hicho kwa upande wa
Zanzibar kimewateua Maryam Ussi Yahaya, Rabia Abdallah, Abdallah Hasnu Makame
na Mohamed Yussuf Nuh.
0 comments:
Post a Comment