Suleiman Msuya
Hamidu Bobali |
MBUNGE wa Mchinga, Hamidu Bobali,
amewasihi wananchi wa jimbo hilo mkoani Lindi kutunza chakula na kujikita
katika kilimo cha mazao yanayovumilia ukame, ili kukabiliana na njaa.
Bobali alisema hayo katika mikutano
mbalimbali aliyofanya hivi karibuni kwenye jimbo hilo kukagua miradi ya
kijamii.
Alisema amelazimika kutoa tahadhari hiyo
mapema kwa sababu hali halisi iliyopo nchini inaonesha mwakani njaa itakuwepo.
Mbunge huyo alisema ipo tabia ya wananchi
kujihusisha na kilimo na baadae kuuza mazao yote jambo linalopaswa kuangaliwa
kwa makini ili wasiathirike baadae.
“Nimelazimika kuwaambia hili hasa nyinyi
wananchi wa kitongoji cha Lichinji, mtunze chakula kwani hii mvua mnayoiona
hapa huko kwengine haipo na mkumbuke kuwa Serikali haitaleta chakula na mimi
sitaweza pia kuleta chakula kwa watu wote,” alisema.
Alisema iwapo kila mwananchi atatunza
chakula alichovuna, ni wazi changamoto ya njaa haitakuwepo hivyo wahakikishe wanauza
chakula kidogo.
Mbunge huyo alisisitiza kwa wananchi wa
mkoa huo kujikita katika kilimo cha mazao yanayovumilia ukame ikiwemo muhogo,
mtama na uwele ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Bobali alisema pamoja na kujikita katika
kilimo hicho, ni wakati muafaka kuanza kuandaa mashamba ya korosho, ili msimu
ukianza wasitumie gharama kubwa.
“Naomba muyape kipaumbele mazao yanayovumilia
ukame kwani kinyume na hivyo tunaweza kuumbuka na msisahau kuanza maandalizi ya
mashamba ya korosho mapema,” alisema.
Alisema zao la korosho limekuwa likipanda
bei kila siku, hivyo matarajio yake ni kuona wananchi wengi waliosusa mashamba
wakirejea na kuyaanda ili wapate mavuno.
Bobali alisema katika hilo hatarajii
kuona propaganda zikipewa nafasi, kwani lengo la wabunge wote wa mkoa huo ni
kuhakikisha bei ya korosho inazidi kupanda kwa kasi ili wakulima wafaidike.
Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa
wakazi wa kitongoji hicho, Ibrahim Tondoro aliunga mkono hoja ya mbunge na
kuwataka wananchi wenzake kujikita katika kilimo chenye tija.
Tondoro alisema ni wazi wananchi
wamekuwa wakisahau na kuuza mazao hivyo angalizo la mbunge litaondoa lawama
ambazo zimekuwa zikitokea kila mara.
0 comments:
Post a Comment