Grace Gurisha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imefuta
kesi ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ya kutoa
lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Sababu ya kufutwa kesi hiyo ni Serikali kushindwa
kupeleka mashahidi mahakamani kwa wakati.
Kesi hiyo ilifutwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi,
Cyprian Mkeha kesi hiyo ilipokuja kusikilizwa mashahidi wa upande wa Jamhuri.
Mkeha aliifuta kesi hiyo chini ya Kifungu cha 225 cha
Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kwa sababu katika miezi 14 ya kesi hiyo
kusikilizwa mahakamani hapo, upande wa Jamhuri ulipeleka shahidi mmoja.
Hakimu alifikia uamuzi huo, baada ya Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Joseph Maugo kuiambia Mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kusikilizwa,
lakini hawakuwa na shahidi, hivyo kuomba ahirisho lingine.
Awali, Askofu Gwajima alikanusha tuhuma za kumtukana Askofu
Pengo, baada ya kusomewa maelezo ya awali (PH) na Wakili wa Serikali, Maugo.
Maugo aliiambia Mahakama kuwa katika tarehe isiyojulikana
kati ya Machi 16 na 25, Askofu Gwajima alitoa mahubiri kwa wafuasi wake, kwenye
viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Dar es Salaam.
Alidai wakati akitoa mahubiri hayo alitoa maneno ya
matusi na ya kumfadhaisha Askofu Pengo, kuwa yeye ni mtoto, mpuuzi na mwenye akili
ndogo sijui amekula nini? Mpuuzi yule, mjinga yule na yeye kuwa anaitwa Askofu
Gwajima.
Wakili huyo alibainisha kuwa Askofu Gwajima wakati anatoa
maneno hayo alirekodiwa kwa video na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Wakati kesi hiyo inasikilizwa, Mahakama hiyo ilikataa
kupokea CD na picha kama kielelezo cha kesi hiyo kwa sababu upande wa Jamhuri ulishindwa
kutimiza vigezo vya kisheria kuwasilisha vilelezo vya elektroniki mahakamani.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, naye alipinga kupokewa
kwa CD hiyo kwa madai kwamba shahidi aliyekuwa anawasilisha hakustahili kwani
siye aliyeitengeneza CD hiyo.
0 comments:
Post a Comment