Zitto Kabwe |
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimelaani
Serikali ya Zambia kumkamata kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha United
Party for National Development (UPND), Hakainde Hichilema ‘HH’ kwa madai ya
uhaini.
Aidha, chama hicho kimesema vitendo
vinavyofanywa na Serikali ya Zambia hasa kwa viongozi wa Upinzani ni ukiukwaji
wa misingi ya demokrasia.
Taarifa hiyo ya kulaani ilitolewa jana na
Katibu wa Mambo ya Nje wa ACT-Wazalendo, John Mbozu akibainisha kusikitishwa na
vitendo vya ukamataji viongozi wa Upinzani katika nchi inayosimamia misingi ya
demokrasia.
Alisema vitendo hivyo vinakwamisha
juhudi za kukuza demokrasia katika bara la Afrika ambalo linapaswa kukubaliana
na mabadiliko ya kidunia.
“Tumelazimika kusema haya kwa sababu
matukio ya ukamataji viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani unaonekana kuota
mizizi na hii haikubaliki na Tanzania vitendo hivyo vipo pia,” alisema.
Alisema ACT-Wazalendo inaomba wapigania
demokrasia, wanaharakati wa haki za binadamu, Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa
Mataifa (UN) kuzungumzia suala hilo.
Alisema katika kupigania haki za
binadamu na heshima ya mtu kokote duniani, chama hicho hakitarudi nyuma ili
haki na usawa viweze kupatikana bila kuangalia dini, rangi na mipaka.
“Watu wote tunahitaji heshima na usawa
kwa mujibu wa sheria kwa kufanya shughuli bila kuvunja sheria,” alisema.
Alisema Hichilema alishiriki uchaguzi
mkuu wa Zambia dhidi ya Rais Edgar Lungu ambapo alimpa wakati mgumu.
Kwa mujibu wa Mbozu, Hichilema alikamatwa
juzi usiku nyumbani kwake New Kasama jijini Lusaka.
Alisema Hichilema atafikishwa mahakamani
kwa tuhuma za uhaini na kwa mujibu wa sheria za Zambia, akipatikana na hatia
atahukumiwa kunyongwa.
Aidha, inasemekana Hichilema hana rekodi
yoyote ya makosa ya jinai na kwamba mashitaka hayo ni ya kutengenezwa ili
kumaliza ndoto zake za kisiasa.
0 comments:
Post a Comment