Leonce Zimbandu
WAJUMBE wawili wa Serikali ya Mtaa wa Mbondole wamezuiwa
kwa siku 90 kujihusisha na shughuli za kiofisi kwa kosa la kupigana ngumi
ofisini.
Imedaiwa kuwa wajumbe hao walifikia hatua kupigana mbele
ya Mwenyekiti wao, Thomas Nyanduli, baada ya mmoja wao kumdhulumu mwenzake posho
ya kushuhudia mauzo ya kiwanja.
Uamuzi huo wa kusimamishwa kazi wajumbe hao ulifikiwa
baada ya Kamati ya Siasa ya CCM iliyoshirikisha matawi manne kuwaita na wao kukiri.
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM wa Matawi hayo, Said
Dikwembe, alisema hayo baada ya kumalizika kwa kikao hicho mwishoni mwa wiki.
Alisema baada ya kupokea taarifa ya wajumbe hao kupigana
mbele ya Mwenyekiti wa Mtaa, aliitisha
kikao cha Kamati ya Siasa ya Chama ili kujadili tukio hilo.
“Tumejadili na kuwaita wajumbe hao ili kutoa utetezi wao
mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa wakakiri
kutenda kosa hilo, hivyo kuwapa onyo,” alisema.
Alisema pamoja na wajumbe kukiri kosa hilo, wajumbe wa Kamati
waliwasimamisha kwa siku hizo 90 ili kutoa fundisho wa watumishi wengine wenye
tabia kama hiyo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Mrisho Jogoo alisema
tukio hilo linaonesha picha mbaya kwa wananchi, iwapo itathibitika kuwa
walidhulumiana.
Alisema hilo ni jambo la ajabu kufanyika katika ofisi ya
Serikali ya Mtaa mbele ya Mwenyekiti wao, kati ya Rehema Bakari na Charles
Mayai.
“Unajua sielewi kwa nini suala hilo halikufika Polisi,
kwani haiwezekani mwanamke kupigana na mwanamume, huo ni udhalilishaji wa
kijinsia,” alisema.
Mmoja wa wajumbe hao, Mayai alikubaliana na uamuzi wa Kamati
ya Siasa, hivyo hawezi kuzungumza lolote.
“Sina cha kuzungumza nakubaliana na uamuzi uliofikiwa na
Kamati,” alisema.
0 comments:
Post a Comment