George Simbachawene |
OFISI ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imewaondoa katika orodha
ya malipo watumishi hewa 13,369.
Akiwasilisha
makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2017/2018 jana
ambapo ameomba jumla ya Sh. trilioni 6.5, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, aliliambia Bunge kwamba
watumishi walioondolewa katika orodha hiyo ni watumishi watoto, wastaafu na
waliofariki.
Simbachawene
alisema watumishi hao hewa wameisababishia Serikali hasara ya Sh. bilioni 25.4
na kati ya fedha hizo Sh. bilioni 2.7 sawa na asilimia 11 zimerejeshwa
serikalini.
Alisema kati
ya watumishi hao, watumishi 541 walikuwa sekritarieti za mikoa12,828 katika mamlaka
za Serikali za Mitaa.
Akizungumzia
kuhusu malalamiko, alisema jumla ya malalamiko 143 kutoka kwa watumishi na
wananchi ambapo yalipatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Simbachawene
alisema hadi kufikia Machi 2017 jumla ya watumishi 102 walichukuliwa hatua
mbalimbali ikiwemo kufukuzwa kazi, kupewa onyo, kuvuliwa madaraka, kushushwa
mshahara, kufikishwa mahakamani na kutakiwa kurejesha fedha zilizopotea.
“Natoa mwito
kwa watumishi wote katika mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza
majukumu yao kwa waledi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea,”alisema.
Kuhusu elimu
bure, Simbachawene alielezea tofauti iliyopo kati ya elimu bure na elimu bila
malipo ambapo alisema kuna tofauti kati ya elimu msingi bure na elimu msingi
bila malipo, akieleza kwamba katika mwaka 2017, jumla ya wanafunzi 3,188,149
waliandikishwa darasa la kwanza.
Waziri huyo
alisema uandikishwaji huo ni sawa na ongezeko la wanafunzi 319,849 ikilinganishwa
na idadi ya wanafunzi hao kwa mwaka 2016, mafanikio ambayo bado ni matokeo
chanya ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa utoaji elimu msingi bila malipo.
0 comments:
Post a Comment