Grace Gurisha
SERIKALI imewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu ikiomba kuwasafirisha Ali Hatibu Haji ‘Shikuba’ na wenzake wawili kwenda
Marekani kukabiliana na tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.
Maombi hayo yaliwasilishwa jana kwa nyakati tofauti na Wakili
wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki akishirikiana na Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Veronica Matikila mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Cyprian Mkeha.
Kakolaki alidai kuwa maombi hayo yalianzishwa na Waziri
wa Katiba na Sheria na kwamba Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alipewa nakala ili
kufuatilia, ambapo aliwasilisha maombi hayo chini ya sheria ya kusafirisha
wahalifu na kuomba yasikilizwe kwa njia ya maneno.
Alidai kuwa maombi hayo ni kwa ajili ya kukamata na kusafirisha
kwenda Marekani wajibu maombi hao watatu kwa ajili ya kujibu mashitaka ya
kujihusisha na dawa za kulevya.
Alitaja wanaotakiwa kusafirishwa kuwa ni Shikuba, Iddi
Mfuru na Tiko Adam. Pia aliomba Mahakama itoe amri ya kuwahifadhi watuhumiwa
wakati wakisubiri kibali cha kuwasafirisha.
Wakili wa Shikuba, Majura Magafu akishirikiana na Hudson
Ndusyepo alieleza kusikia maombi ya upande wa mashitaka na akaomba wapewe muda.
Magafu alidai kuwa suala la kumtoa raia wa nchi nje ya nchi si suala rahisi.
Kwa sababu walishafikishwa mbele ya Mahakama aliomba
ahirisho ili kupata nafasi ya kupitia makabrasha waliyopewa. Alibainisha kuwa
makabrasha hayo ni hati ya ushahidi ambao unatarajiwa kutolewa nje ya nchi.
Hakimu Mkeha aliipanga kesi hiyo ije leo kwa ajili ya kusikiliza
maombi hayo.
0 comments:
Post a Comment